Lugha Nyingine
Rais Xi atuma pongezi kwa Rais wa Misri kwa ufunguzi wa Jumba la Makumbusho Kuu la Misri
BEIJING - Rais Xi Jinping wa China ametuma ujumbe wa pongezi kwa mwenzake wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi kwa ufunguzi wa Jumba la Makumbusho Kuu la Misri, ambapo katika ujumbe wake huo alioutuma Jumamosi, Rais Xi ametoa pongezi zake za dhati kwa Rais Sisi na watu wa Misri wakati jumba hilo la makumbusho likifunguliwa.
Rais Xi amesema anaamini kwamba Jumba hilo litaacha alama kubwa katika historia ya kitamaduni ya Misri na kubeba jukumu muhimu katika kuhifadhi na kurithisha ustaarabu wa kale wa Misri.
Amesema kuwa China na Misri zina urafiki wa muda mrefu, na ushirikiano wao wa kimkakati wa pande zote umekuwa ukistawi katika miaka ya hivi karibuni.
“Nchi hizi mbili zimekuwa zikifurahia mawasiliano ya kati ya watu na ya kitamaduni yenye hamasa kubwa na ya aina mbalimbali,” Rais Xi amesema, akiongeza kuwa maonyesho makubwa ya mabaki ya kale ya Misri yalifanyika kwa mafanikio katika Jumba la Makumbusho la Shanghai na kwamba timu ya pamoja ya kiakiolojia ya China na Misri kwa sasa inafanya kazi pamoja chini ya mapiramidi huko Saqqara kutafiti na kuchunguza maajabu yasiyofahamika ya ustaarabu wa kale wa Misri.
Rais Xi amesema inatia moyo kuona nchi hizo mbili zenye ustaarabu wa kale zikiwasiliana kuungana mkono, huku watu wa nchi hizo mbili wakizidi kuwa karibu zaidi kupitia maelewano na uhusiano wa karibu.
“Huku dunia ya leo ikipitia mabadiliko ya kasi ambayo hayajawahi kuonekana katika miaka 100 iliyopita, China na Misri, zote zikiwa nchi zenye ustaarabu wa kale, zinapaswa kuendelea kuzidisha mawasiliano na hali ya kufunzana miongoni mwa ustaarabu tofauti, kuingiza msukumo mpya kwenye maendeleo ya ushirikiano wao kimkakati wa pande zote, na kuchangia nguvu za ustaarabu katika ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu,” ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



