Lugha Nyingine
Misri yafungua Jumba Kuu la Makumbusho la Misri, yatarajia kustawisha utalii na kuinua uchumi
Wasanii wakifanya maonesho ya michezo ya sanaa kwenye sherehe ya kufunguliwa kwa Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM) huko Giza, Misri, Novemba 1, 2025. (Xinhua)
CAIRO - Kufunguliwa rasmi kwa Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM) kunatarajia kustawisha sekta ya utalii ya nchi hiyo na kuingiza msukumo mpya katika uchumi wake, wataalam wa utalii wamesema, wakati ambapo jumba hilo alama lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu likiongeza kivutio kipya kwa mazingira ya kitamaduni ya Misri.
Mohamed Othman, mkuu wa Kamati ya Masoko ya Utalii wa Utamaduni katika Misri ya Juu, amesema kufunguliwa kwa jumba kuu hilo si kama tu kumeonesha jumba hilo ni Mnara wa Utamaduni bali pia ni kichocheo cha ufufukaji wa shughuli za utalii wa kitamaduni, ambalo litasaidia kuongeza muda wa wageni kubaki nchini humo, na kusaidia Misri kusonga mbele kuelekea kutimiza lengo lake la kuvutia watalii milioni 30 kwa mwaka katika miaka kadhaa ijayo.
Jumba kuu hilo la makumbusho limejengwa kwenye Uwanda wa Giza, umbali wa kilomita 2 tu kutoka kwenye Mapiramidi na Sphinx, eneo lake limefikia mita za mraba takriban 500,000, na kulifanya kuwa jumba kubwa zaidi la makumbusho duniani lenye mada pekee ya ustaarabu.
Baada ya kufanya ujenzi kwa muda wa miongo miwili, jumba hilo lililogharimiwa kwa dola bilioni limefunguliwa rasmi juzi Jumamosi jioni katika sherehe iliyohudhuriwa na makumi ya ujumbe wa kimataifa, wakiwemo ujumbe wa wakuu wa nchi na serikali.
Picha hii iliyopigwa Novemba 1, 2025 ikionyesha onyesho la droni na mwanga kwenye hafla ya kufunguliwa kwa Jumba kuu la Makumbusho la Misri (GEM) huko Giza, Misri. (Xinhua/Ahmed Gomaa)
Jumba hilo la makumbusho lina mabaki ya kale ya utamaduni zaidi ya 100,000 yanayojumuisha maelfu ya miaka ya historia ya Misri, ikiwemo sanamu ya Mfalme Ramses II yenye urefu wa mita 12, na umri wa miaka 3,200. Jumba kuu hili likitazamana na mapiramidi, usanifu wake kiishara unaunganisha jumba hilo alama mpya ya kihistoria na mapiramidi, ambayo ni maajabu ya mwisho yaliyobakia ya Dunia ya kale.
Picha hii iliyopigwa Februari 21, 2024 ikionyesha Hekalu Kubwa la Abu Simbel lililowashwa taa zake huko Aswan, Misri. (Xinhua/Sui Xiankai)
Sekta ya Utalii ni moja ya vyanzo vikuu vya fedha za kigeni vya Misri, pamoja na pesa zinazotumwa na Wamisri kutoka ng’ambo, mapato ya Mfereji wa Suez, na mauzo ya nje. Sekta hiyo imeendelea kufufuka licha ya hali ya kukosa utulivu wa kikanda.
Takwimu rasmi zlizotolewa zimeonesha kuwa, mapato yatokanayo na shughuli za utalii yalifikia dola za Kimarekani bilioni 15.3 mwaka 2024,ambayo ni ongezeko la asilimia 9 kuliko mwaka uliopita, huku idadi ya watalii wanaoingia nchini humo ikiongezeka kwa asilimia 5 hadi kufikia milioni 15.7. Serikali inalenga kuvutia watalii wapatao milioni 18 mwaka 2025.
Kwenye sherehe ya kufunguliwa kwa jumba hilo, waziri wa Utalii na Mabaki ya Kale ya Utamaduni wa Misri Sherif Fathy alisema jumba hilo la makumbusho linatarajiwa kuvutia watalii wapatao 15,000 kwa siku, au takriban milioni 5 kwa mwaka, na kulifanya kuwa kichocheo kikubwa zaidi cha ukuaji wa utalii wa siku za baadaye.
Watalii wakitembelea Jumba Kuu la Makumbusho la Misri wakati wa uendeshaji wa majaribio huko Giza, Misri, Juni 12, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomma)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



