Lugha Nyingine
Botswana yaunga mkono kuanzishwa kwa Mfuko wa Bioanuwai wa Afrika kwa ajili ya ufadhili wa uhifadhi

Rais wa Botswana Duma Boko akizungumza kwenye Mkutano wa kwanza wa Bioanuwai wa Afrika mjini Gaborone, Botswana, Novemba 5, 2025. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
GABORONE - Rais Duma Boko wa Botswana akizungumza jana Jumatano kwenye Mkutano wa kwanza wa Bioanuwai wa Afrika uliofanyika Gaborone, mji mkuu wa Botswana, ametangaza kwamba nchi yake inaunga mkono Mfuko wa Bioanuwai wa Afrika na kuhimiza nchi za Afrika kubadilisha muundo wao wa kiuchumi ili kuzingatia thamani ya mazingira ya asili na kukabiliana na upungufu mkubwa wa fedha za uhifadhi.
Rais Boko amehimiza nchi za Afrika kuhakikisha kwamba thamani ya bioanuwai imejumuishwa katika mipango ya kiuchumi, mikakati ya maendeleo, na mifumokazi ya utawala.
“Kupotea kwa bioanuwai, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa ardhi, kupungua kwa misitu, uhaba wa maji, kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, njia zinazokatika kwa wanyamapori, na uvamizi wa spishi zisizo asilia vinatishia ustawi na usalama wa jamii,” amesema.
Rais huyo amesema, ustawi lazima utambuliwe si tu kwa pato la jumla la taifa, bali pia kwa mifumo salama ya chakula, maji safi, jamii himilivu, na mifumo mizuri ya ikolojia ambayo inazuia athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza kwamba Afrika inabeba mapengo makubwa katika ufadhili wa uhifadhi. Kwa hivyo, Botswana inaunga mkono kuanzishwa kwa Mfuko wa Bioanuwai wa Afrika ili kuziba pengo hilo.
Rais Boko pia ametoa wito wa juhudi za pamoja za kuhamasisha rasilimali za ndani ya Afrika na za kimataifa, kuhimiza uwekezaji binafsi, na kuchunguza zana za kivumbuzi kama vile dhamana za kijani na mikopo ya bioanuwai.
Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Selma Malika Haddadi amesema AU ina nia ya kusaidia nchi wanachama wake kutekeleza Mkakati wa Bioanuwai wa AU na kuulinganisha na malengo ya bara na ya kimataifa.
Ukiwa umefanyika chini ya kaulimbiu ya “Kutumia Ipasavyo Bioanuwai kwa Ustawi wa Afrika”, mkutano huo uliofanyika kuanzia Novemba 2 hadi Novemba 5, umemalizika kwa kupitishwa kwa Azimio la Mkutano wa Bioanuwai wa Afrika.
Mkutano huo umetumika kama jukwaa la bara hilo kwa ajili ya kuoanisha vipaumbele vya Afrika chini ya Mfumokazi wa Bioanuwai wa Kunming-Montreal na kusukuma mbele utekelezaji wa Mkakati wa Bioanuwai wa AU.

Rais Duma Boko wa Botswana (wa tatu, kulia), Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Selma Malika Haddadi (wa pili, kulia) wakishiriki kwenye Mkutano wa kwanza wa Bioanuwai wa Afrika mjini Gaborone, Botswana, Novemba 5, 2025. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



