Waziri Mkuu wa China kuhudhuria mkutano wa SCO, mkutano wa viongozi wa G20 na kufanya ziara Zambia

(CRI Online) Novemba 14, 2025

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetangaza jana Alhamisi kwamba Waziri Mkuu wa China Li Qiang atahudhuria Mkutano wa 24 wa Baraza la Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) mjini Moscow Novemba 17 na 18 kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin.

Msemaji wa wizara hiyo Lin Jian amesema kuwa, baada ya hapo Li atafanya ziara rasmi nchini Zambia Novemba 19 na 20 kwa mwaliko wa serikali ya Jamhuri ya Zambia.

Ameongeza kuwa, waziri mkuu huyo pia atahudhuria Mkutano wa 20 wa G20 utakaofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia Novemba 21 hadi 23 kwa mwaliko wa serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo ujao wa SCO, Lin amesema wakati wa Mkutano wa SCO wa Tianjin, viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo walifikia maelewano muhimu mfululizo ya pamoja kuhusu kudumisha Moyo wa Shanghai na kuhimiza maendeleo na mageuzi ya SCO, na kuongoza jumuiya hiyo katika hatua mpya ya maendeleo bora yenye mshikamano, uratibu, nguvu na tija kubwa zaidi.

Aidha kuhusu ziara ya Zambia Bw. Lin amesema China inatarajia kushirikiana na Zambia kupitia ziara hiyo ili kuharakisha utekelezaji wa maelewano muhimu ya pamoja yaliyofikiwa na marais wa nchi hizo mbili na matokeo ya Mkutano wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Kuhusu mkutano wa G20, Lin amefafanua kuwa China inaiunga mkono Afrika Kusini ambayo ni mwenyekiti wa zamu wa G20 na iko tayari kushirikiana na pande mbalimbali chini ya kaulimbiu ya "Mshikamano, Usawa, Uendelevu" ili kujenga makubaliano ya kuunga mkono ushirikiano wa pande nyingi, kujenga uchumi wa dunia ulio wazi na kuhimiza ushirikiano wa kimaendeleo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha