Lugha Nyingine
Panda waleta upendo kwenye maisha ya kila siku mjini Berlin, Ujerumani
Panda Leni (kushoto) na Lotti, wanaojulikana kwa majina ya kichina ya Meng Hao na Meng Tian, wakionekana kwenye Bustani ya Wanyama ya Berlin mjini Berlin, Ujerumani, Agosti 22, 2025. (Xinhua/Du Zheyu)
BERLIN – Miaka karibu 40 iliyopita, Andreas Knieriem alimwona panda kwa mara ya kwanza ambapo katika mwanga laini wa alasiri, panda huyo mgeni mwenye rangi za mweusi na mweupe alikuwa amekaa kimya, akitafuna mianzi kwa utulivu.
"Wakati wowote unapomwona panda, huwezi kujizuia kutabasamu. Ni mwororo na mpole, taswira halisi ya wema wa maumbile." Andreas Knieriem, ambaye sasa ni mkuu wa bustani hiyo amesema.
Panda huyo aliyeonwa kwa mara ya kwanza na Knieriem aliitwa Bao Bao. Mwaka 1980, panda huyo dume mwenye umri wa miaka miwili na mwenzake Tian Tian walifika Berlin kama "mabalozi wa urafiki" kutoka China. Bao Bao alipofariki Berlin akiwa na umri wa miaka 34, alikuwa panda dume aliyekuwa akiishi kwa miaka mingi zaidi katika mazingira ya kufugwa.
"Bao Bao aliambatana na vizazi vya wakazi wa Berlin," Knieriem amesema, akiongeza kuwa kwa watu wengi mjini humo, panda huyo hakuwa tu nyota mkubwa wa bustani hiyo, lakini pia ishara ya urafiki kati ya Ujerumani na China.
Miaka kadhaa baadaye, Knieriem amesema bado anaweza kuona dalili za Bao Bao katika kila panda anayekwenda Berlin. Mwaka 2017, panda Meng Meng na Jiao Qing walifika kutoka mji wa Chengdu kusini magharibi mwa China, ambao ni nyumbani kwa panda wengi.
Panda pacha vichanga Meng Hao (kushoto) na Meng Tian wakionekana kwenye Bustani ya Wanyama ya Berlin mjini Berlin, Ujerumani, Desemba 6, 2024. (Xinhua/Du Zheyu)
Agosti 2019, Meng Meng alizaa pacha wa kwanza wa panda nchini Ujerumani, Meng Xiang na Meng Yuan, ambao pia wanajulikana kwa Wajerumani kwa majina ya Pit na Paule. Panda hao ndugu walirudi China mwaka 2023. Mwaka uliofuata, Agosti 22, 2024, Meng Meng alijifungua tena, mapacha wa kike Meng Hao na Meng Tian, ambao pia walipewa majina ya Kijerumani: Leni na Lotti.
Kuzaliwa huko kulichochea tena "upendo wa panda" mjini Berlin, Knieriem amesema. Siku ambayo watoto hao wawili walionyeshwa kwa mara ya kwanza, umati mkubwa wa watu ulijipanga foleni kwa saa nyingi, huku foleni ikiendelea mamia ya mita nje ya bustani ya panda.
Lisa Fuersch, mmoja wa watunza panda wa bustani hiyo ya wanyama, bado anakumbuka siku za mwanzo za watoto hao.
"Vilipozaliwa, vilikuwa na urefu wa sentimita 14 na uzito wa gramu zaidi ya 100 tu," amesema.
Panda Meng Xiang (juu) akicheza na Meng Yuan kwenye Bustani ya Wanyama ya Berlin mjini Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, Agosti 31, 2023. (Xinhua/Ren Pengfei)
Kwa Knieriem, uzoefu huo pia umeonyesha nguvu ya ushirikiano. Wataalamu wa China walikaa Berlin kwa angalau miezi minane, ili kutoa msaada muhimu katika uzazi na utunzaji wa mapacha wa pili.
"Kuanzia ufuatiliaji wa uzazi na uchambuzi wa homoni hadi utunzaji wa watoto wa panda -- kila hatua ni kazi ya timu," Knieriem ameelezea, akiongeza: "Ushirikiano umekuwa mzuri sana. Tunajifunza kutoka kwa kila mmoja na kukua pamoja."
Mtunzaji panda akimsaidia panda kujifunza kupanda kwenye kituo cha panda cha Shenshuping cha Hifadhi ya Taifa ya Mazingira ya Asili ya Wolong, Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, Novemba 6, 2025. (Xinhua/Xu Bingjie)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



