Israeli yafungua tena eneo la kuvuka mpaka la Zikim ili kuruhusu malori ya vitu vya msaada kuingia Gaza Kaskazini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 14, 2025

JERUSALEM - Israeli ilisema Jumatano kuwa imefungua tena eneo la kuvuka mpaka la Zikim ili kuruhusu malori ya vitu vya msaada wa kibinadamu kuingia Gaza Kaskazini ambapo taarifa kutoka ofisi ya Mratibu wa Shughuli za Serikali katika Mipaka (COGAT) imesema kwamba eneo hilo la kuvuka mpaka limefunguliwa kwa ajili ya kuingia kwa malori ya vitu vya msaada wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo kutoka COGAT, ambayo ni chombo chini ya Wizara ya Ulinzi ya Israeli kinachohusika na kutekeleza sera za mambo ya raia na ubinadamu za serikali katika maeneo ya Palestina imeongeza kuwa msaada huo utawasilishwa kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa baada ya kufanyiwa "ukaguzi wa kina wa usalama" na Mamlaka ya Maeneo ya Kuvuka Mpaka ya Nchikavu ya Wizara ya Ulinzi, na hatua hiyo imefuata "maagizo ya ngazi ya kisiasa."

Katika muda mrefu uliopita, Umoja wa Mataifa na mashirika ya msaada wa kimataifa yamekuwa yakiihimiza Israeli kufungua tena maeneo ya kuvuka mpaka kuelekea kaskazini mwa Gaza ili vitu zaidi viweze kufika katika eneo hilo lililoathiriwa sana na vita.

Ofisi kuu ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Ubinadamu ilisema katika taarifa mpya ya kuelezea hali ya mambo mwishoni mwa Oktoba kwamba "kufunguliwa kwa maeneo ya kuvuka mpaka ya kuelekea moja kwa moja kaskazini ni muhimu sana kwa kuhakikisha vitu vya msaada vinawasilishwa kwa watu haraka iwezekanavyo."

Maofisa hao wa mambo ya ubinadamu wanasema uwasilishaji wa vitu vya msaada kwa Gaza umekuwa ukizuiliwa kutokana na ukaguzi mkali wa usalama wa Israeli na vizuizi vikali kwa bidhaa zinazoruhusiwa.

Wamesema, hata baada ya malori kuingia katika eneo hilo, usambazaji wa mahitaji bado ni mgumu kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu na hatari ya uporaji.

Makubaliano ya kusimamisha vita ambayo yalianza Oktoba 10 hayajasimamisha kabisa mashambulizi ya Israeli huko Gaza, huku vikosi vya Israeli vikiendelea na ubomoaji katika maeneo yaliyo chini yao. Takwimu zilizotolewa na idara za afya za Gaza zimeonesha kuwa, Watu zaidi ya 245 wameuawa tangu makubaliano ya hayo ya kusimamisha vita yalipoanza, na kusababisha idadi ya jumla ya vifo vya watu imefikia 69,185 kutokana na mashambulizi ya Israeli tangu Oktoba 7, 2023.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha