Lugha Nyingine
Japan lazima iondoe kauli zake zinazohusiana na Taiwan, la sivyo ibebe matokeo yote: Wizara ya Mambo ya Nje ya China
BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Lin Jian amesema jana Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba, Japan lazima mara moja isahihishe makosa yake na kuondoa kauli zake zisizo na msingi kuhusu Taiwan ya China, vinginevyo, matokeo yote yatakayotokea lazima yabebwe na Japan.
Lin ameyasema hayo akijibu swali kuhusu Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi ambaye hivi karibuni alisema kwamba "matumizi ya nguvu dhidi ya Taiwan" ya China Bara yanaweza kuwa "hali inayotishia usalama" wa Japan. Waziri mkuu huyo amekataa kuondoa kauli yake hiyo inayoashiria uwezekano wa kuingilia kati kijeshi kwenye Mlango-Bahari wa Taiwan.
"Hiyo inawakilisha kuingilia kati waziwazi mambo ya ndani ya China, kupinga maslahi ya msingi ya China, na kukiuka mamlaka ya China. China inapinga vikali na kamwe haitavumilia kauli kama hizo," Lin amesema.
"Jaribio la kiongozi huyo wa Japan kuingilia masuala ya pande mbili za Mlango Bahari wa Taiwan ni dharau kubwa kwa haki ya kimataifa, uchochozi wa wazi kwa utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, na pigo kubwa kwa uhusiano kati ya China na Japan," amesema.
"Kama Japan itathubutu kuingilia kati mambo ya pande mbili za Mlango Bahari wa Taiwan, itakuwa kitendo cha uchokozi na hakika itakabiliwa na majibu thabiti kutoka kwa China," amesema, na kuongeza kuwa, "Tutatumia kwa dhati haki yetu ya kujilinda chini ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa na kutetea mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya China."
Msemaji huyo wa China ameionya Japan dhidi ya kucheza na moto kuhusu suala la Taiwan. "Wale wanaocheza na moto wataungua wenyewe!" Lin amesema.
Lin amesema kuwa licha ya malalamiko makali na upingaji rasmi wa China, Takaichi bado amekataa kubadili msimamo na kuondoa kauli alizotoa.
"Kauli hizo potofu zinakiuka kwa kiasi kikubwa kanuni ya kuwepo kwa China moja, kanuni elekezi zilizowekwa katika nyaraka nne za kisiasa kati ya China na Japan, na kanuni za kimsingi za uhusiano wa kimataifa," ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



