Idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar, Tanzania yaongezeka kwa asilimia 24 mwezi Oktoba

(CRI Online) Novemba 14, 2025

Visiwa vya Zanzibar, Tanzania vimeshuhudia watalii 86,740 waliofika mwezi Oktoba mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.2 kutoka 69,860 mwezi huohuo mwaka jana.

Hayo yametangazwa na afisa wa utafiti na takwimu katika Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, Hassan Ameir Vuai kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Alhamisi akisema idadi hiyo pia imeonyesha ongezeko la asilimia 3.1 kutoka wageni 84,154 waliorekodiwa mwezi wa Septemba mwaka 2025.

Vuai amesema Ulaya bado inaendelea kuwa chanzo kikuu cha utalii wa visiwa hivyo, ikichukua asilimia 67.2 ya jumla ya watalii wote, ikifuatiwa na Afrika, Asia, na Oceania.

Italia imeongoza kwenye orodha ya nchi kwa kurekodi watalii 8,894 waliofika, ikichukua asilimia 10.3 ya jumla, ikifuatiwa na Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, na Afrika Kusini.

Ameongeza kuwa asilimia 92 ya watalii hao waliingia kwenye visiwa hivyo kwa ndege na asilimia 8 kwa njia ya bahari.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha