Lugha Nyingine
Reli ya TAZARA yaingia katika ukurasa mpya wa urafiki kati ya China na Afrika
LUSAKA "Habari! Rafiki yangu Mchina!" Kwenye reli katika Stesheni ya Reli ya New Kapiri Mposhi katika Jimbo la Kati la Zambia, mhandisi wa ujenzi Stanley Simushi alimsalimia mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la China, Xinhua kwa lugha fasaha ya Kichina.
Simushi alinyoosha kidole kuonesha kundi la wafanyakazi wakibadilisha mataruma kwenye sehemu ya reli ndani ya stesheni hiyo. Kwa kutumia spana na bisbisi, wafanyakazi hao walikuwa wakiondoa nati na misumari, wakiinua reli na kufunga mataruma mapya.
New Kapiri Mposhi ni stesheni ya mwisho ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ambayo inaelekea mashariki kutoka Dar es Salaam, Tanzania, hadi stesheni hiyo ya Zambia. Reli hiyo ilijengwa kwa mikopo isiyo na riba kutoka China na kukabidhiwa rasmi kwa serikali za Tanzania na Zambia Julai 14, 1976.
Ndani ya stesheni hiyo kuna mnara unaandika urefu wote wa reli: kilomita 1,860.54369. Urefu huo wa reli kwa usahihi unaonyesha juhudi za wahandisi na wafanyakazi wa ujenzi wa China zaidi ya 50,000 ambao, kwa zaidi ya miaka mitano na miezi minane, walifanya kazi pamoja na wenzao wa Tanzania na Zambia kwa jasho, damu na kujitoa muhanga kukamilisha reli hiyo.
Septemba 4, 2024, viongozi wa nchi hizo tatu walishuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya maelewano kuhusu mradi wa ufufuaji wa reli hiyo ya TAZARA.
Huku mradi huo ukisonga mbele, uwezo wa kubeba mzigo wa reli hiyo unatarajiwa kufikia tani milioni 2.4 kwa mwaka, na muda wa usafirishaji unaweza kupunguzwa kwa karibu theluthi mbili.
"Njoo, nitakupeleka kwenye karakana ya injini za treni. Kuna injini za Kichina huko," amesema dereva wa treni Jackson Masase, ambaye amekuwa akifanya kazi katika stesheni hiyo kwa miaka 20. Amesema injini za treni katika stesheni hiyo zinatoka nchi tofauti, "lakini zile za Kichina ndizo bora zaidi -- zina nguvu na za kuaminika."
Alimwonyesha mwandishi wa habari chumba cha dereva, akionyesha bamba lenye maelezo ya kampuni ya China iliyounda injini hiyo. Mkuu wa Stesheni hiyo Mukololo Chanda baadaye alisema kilichomvutia zaidi ni kuona namna TAZARA ilivyoleta urahisi na nguvu hai kwa wakazi wa pembezoni mwa reli hiyo, akiongeza kuwa reli hiyo imesaidia kuzidisha urafiki na wenzake wengi wa China.
Umbali wa kilomita takriban 20 kaskazini mashariki mwa Lusaka, Bustani ya Ukumbusho ya TAZARA inahifadhi kumbukumbu za pamoja za watu wa China, Tanzania na Zambia. "Siku zote nimekuwa nikiguswa sana ninapoingia hapa," amesema mfanyakazi Tobias Lingweshi.
Wakati wa ujenzi wa reli hiyo na miradi ya ushirikiano inayohusiana nayo, wafanyakazi 69 wa China walipoteza maisha yao -- 18 kati yao walifariki wakiwa Zambia. Vifaa, mali na picha zao za rangi nyeusi na nyeupe zinaonyeshwa kwenye bustani hiyo, zikirekodi kipindi chenye mambo magumu na azimio.
Karibu nusu karne baadaye, "Barabara hiyo ya Chuma" ambayo inabeba uhusiano mkubwa kati ya China, Tanzania na Zambia inaingia katika hatua mpya ya ufufuaji.
Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Zambia, Frank Tayali, amesema ufufuaji wa reli hiyo unaendana na maono ya serikali ya kuwa taifa lililounganishwa na ardhi na kituo cha usafirishaji kusini na kati mwa Afrika.
Reli hiyo, inayojulikana kwa jina la "barabara ya uhuru," inatarajiwa kuchochea biashara ya kikanda, kutoa ajira na kuunga mkono ustawi wa pamoja.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




