Lugha Nyingine
UN-Habitat yatoa tena wito wa ukuaji endelevu wa miji katika nchi za Kusini

Picha iliyopigwa Novemba 25, 2025, ikionyesha mwonekano wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 13 wa Jukwaa la Miji Duniani, uliopangwa kufanyika Baku, Azerbaijan Mei 2026, jijini Nairobi, Kenya. (Xinhua/Han Xu)
NAIROBI – Dira mpya kwa ajili ya kuimarisha uhimilivu wa miji inayokua kwa kasi katika nchi za Kusini huku kukiwa na changamoto nyingi inapaswa kutekelezwa kupitia makubaliano miongoni mwa wadau muhimu, Anaclaudia Rossbach, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Makazi ya Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) amesema jana Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya.
Rossbach amesema kuwa Nchi za Kusini ni kitovu kipya cha ukuaji wa haraka wa miji, hivyo kuna hitaji la kuanzisha hatua za kisera na za kisheria ili kuhakikisha miji ni ya kijani na inayofaa kwa watu kuishi.
Amesema ukuaji wa miji katika nchi zinazoendelea umeambatana na changamoto nyingi, kama vile ukuaji wa makazi yasiyo rasmi, umaskini na hali ya ukosefu wa usawa, ubaguzi, na ukosefu wa huduma za msingi.
Rossbach amesema kuwa, kama yatasimamiwa vizuri, maendeleo ya ukuaji wa miji yanaweza kuchochea ukuaji, uvumbuzi, na mageuzi ya kijamii barani Afrika, Amerika Kusini, na Asia ambayo inakadiriwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu mijini duniani ifikapo mwaka 2050.
Afisa huyo wa UN-Habitat ametoa maoni hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa 13 wa Jukwaa la Miji Duniani, uliopangwa kufanyika Baku, Azerbaijan Mei 2026, chini ya kaulimbiu ya "Kuipa Dunia Makazi: Miji na Jamii Salama na Himilivu."
Rossbach amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, Jukwaa la Miji Duniani limekuwa mkutano mkuu kwa wadau muhimu, wakiwemo mawaziri, mameya, wavumbuzi, watendaji wa asasi za kiraia, wawekezaji, na wasomi, ili kufufua ajenda ya maendeleo ya ukuaji wa miji.
Rossbach ameongeza kuwa, Ajenda Mpya ya Miji inatoa wito kwa mipango ya miji inayotoa kipaumbele kwa watu, kuboresha makazi yasiyo rasmi na uhimilivu wa kiikolojia wa miji - vipaumbele ambavyo ni muhimu kwa ukuaji endelevu wa miji katika Nchi za Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



