Lugha Nyingine
Kenya yatoa wito wa kulinda shule dhidi ya matishio ya kidigitali na migogoro
Kenya imetoa wito jana Jumanne kwa jumuiya ya kimataifa kulinda usalama wa elimu dhidi ya matishio ya migogoro na ya kidigitali.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni waziri anayeshughulikia mambo ya nje na masuala ya diaspora wa Kenya Bw. Musalia Mudavadi wakati akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Kimataifa kuhusu Maazimio ya Shule Salama, ambapo ametahadharisha kuwa usalama wa shule hautishiwi na migogoro ya kisilaha tu, bali pia kwa kuongezeka kwa hatari za mtandao wa intaneti, ulaghai wa kisaikolojia na AI.
Bw. Mudavadi ametoa wito kwa wadau husika duniani kupanua uelewa wao kuhusu ukosefu wa usalama akieleza kuwa AI na majukwaa ya kidigitali vimefungua njia mpya za kuenea kwa taarifa potoshi, uonevu mtandaoni, kuenezwa kwa mirengo yenye itikadi kali na unyonyaji miongoni mwa wanafunzi.
Pia ametoa wito kwa serikali, asasi za kiraia, wasomi na kampuni za teknolojia kushirikiana kulinda wanafunzi shuleni kupitia mageuzi ya sera, mifumo ya usalama wa intaneti, miradi ya elimu ya kidigitali na mafunzo kwa walimu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



