Treni za mizigo za China-Ulaya zageuza kituo cha samani cha ndani kuwa mshiriki wa biashara duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 26, 2025

NANCHANG - Miaka mitano iliyopita, Zhu Hao, meneja mkuu wa masoko wa Kampuni ya Samani ya Jiangxi Sanyou katika Mkoa wa Jiangxi, mashariki mwa China, hakuweza kufikiria kwamba soko la Ulaya siku moja litakuja kuwa mteja wake mkuu. Hata hivyo, leo, Ulaya inachukua asilimia 70 ya oda za nje za kampuni hiyo.

Mageuzi hayo yalianza kwa ziara ya ujumbe kutoka Hungary uliowezeshwa na Bandari Kavu ya Kimataifa ya Ganzhou. Oda yenye thamani ya yuan 100,000 (dola za Kimarekani 14,119.1) iliwekwa na kusafirishwa kupitia treni za mizigo za China-Ulaya.

"Samani hizo zilifika Hungary ndani ya siku 20 tu, chini ya nusu ya muda unaohitajika kwa usafirishaji wa majini," Zhu amesema, akielezea kwamba tangu wakati huo, kampuni hiyo imeanzisha ushirikiano thabiti na wateja nchini Hungary, Ujerumani na Poland. Mwaka jana, oda zake za Ulaya, zote zikisafirishwa kupitia huduma hiyo ya treni za mizigo za China-Ulaya, zilizidi yuan milioni 7.

"Kwetu sisi, treni za mizigo za China-Ulaya si tu reli ya kiunganishi kati ya Asia na Ulaya; ni njia ambayo ukuaji na fursa zetu zinapatikana," Zhu ameongeza.

Kampuni hiyo ipo katika Eneo la Nankang la Mji wa Ganzhou, linalojulikana kwa jina la "mji mkuu wa samani za mbao ngumu wa China." Eneo hilo lina kampuni za kutengeneza samani na kampuni zinazounga mkono sekta hiyo zaidi ya 10,000, zikiwaajiri watu 500,000.

Hapo awali, mizunguko mirefu ya usafirishaji wa majini ya siku 45 hadi 60 ilifanya kuhudumia soko la Ulaya kuwa na changamoto. Uzinduzi wa huduma za treni za mizigo za China-Ulaya umebadilisha hali hiyo siku hadi siku.

Tangu treni ya kwanza ya mizigo ya China-Ulaya ilipoondoka kutoka Jiangxi mwishoni mwa mwaka 2015, Bandari kavu hiyo ya Kimataifa ya Ganzhou, bandari kavu pekee katika mkoa wa Jiangxi na eneo la zamani la mapinduzi la China, imeendesha treni zaidi ya 1,700 kama hizo, ikijenga mtandao wa usafirishaji unaofika Asia na Ulaya.

Kutokana na huduma hiyo, mbao huagizwa kutoka nchi na maeneo zaidi ya 50, huku bidhaa za samani zikisafirishwa kwenda nchi na maeneo zaidi ya 100 duniani kote.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu treni za mizigo za China-Ulaya, hadi kufikia Oktoba 2025, huduma hiyo ilikuwa imefanya safari 118,600, zikisafirisha makotena milioni 11.7 (TEUs), kufikia miji 232 katika nchi 26 za Ulaya. Hadi kufikia mwisho wa 2024, jumla ya thamani ya bidhaa zilizosafirishwa ilikuwa imefikia dola za Marekani bilioni 426.4.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha