Rais Xi atoa salamu za pongezi kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 27, 2025

BEIJING - Rais Xi Jinping wa China ametuma salamu za pongezi kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika juzi Jumanne kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina.

Katika ujumbe wake huo, Rais Xi amesema kwamba suala la Palestina ndio kiini cha mgogoro wa Mashariki ya Kati, likiathiri haki na usawa wa kimataifa, na utulivu wa kikanda.

Ameongeza kuwa katika hali ya sasa, jumuiya ya kimataifa inapaswa kujenga maafikiano makubwa zaidi na kuchukua hatua za kijasiri zaidi ili kuhakikisha usimamishaji mapigano wa pande zote na wa kudumu katika Gaza na kuzuia kuibuka tena kwa mgogoro.

Huku akisema kuwa utawala na ujenzi upya wa Gaza baada ya mgogoro unapaswa kufanyika chini ya kanuni ya "Wapalestina kutawala Palestina," kwa kuheshimu kikamilifu matakwa ya watu wa Palestina na kuzingatia mambo halali ya msingi yanayofuatiliwa na nchi katika eneo hilo, Rais Xi amesisitiza umuhimu wa kuboresha haraka hali ya kibinadamu katika Gaza na kupunguza mateso ya watu wa Palestina.

Amesema, la muhimu zaidi ni kwamba juhudi zinapaswa kuimarishwa katika kutafuta suluhisho la nchi mbili ili kuhimiza utatuzi wa mapema wa kisiasa wa suala la Palestina.

Rais Xi amesisitiza kwamba suala la Palestina pia ni jaribio la ufanisi wa mfumo wa uongozi duniani. Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukabiliana na mzizi wa sababu za suala la Palestina, kubeba wajibu, kuchukua hatua madhubuti, kurekebisha dhuluma za kihistoria, na kulinda haki na usawa.

"Ikiwa ni nchi mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, China inaunga mkono kithabiti harakati ya haki ya watu wa Palestina kurejesha haki zao halali za kitaifa," Rais Xi amesema, akiongeza kuwa China itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kufanya juhudi zisizokoma kwa ajili ya utatuzi wa pande zote, wa haki na wa kudumu wa suala la Palestina mapema.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha