Viongozi wa AU na EU waahidi ushirikiano wa karibu zaidi kwenye mkutano wa kilele wa Luanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 27, 2025

LUANDA - Viongozi wa Afrika na Ulaya wamesisitiza ahadi yao ya kuimarisha ushirikiano katika amani na usalama, maendeleo, hatua za mabadiliko ya tabianchi na wahamiaji kwenye Mkutano wa 7 wa Viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliofanyika Luanda, mji mkuu wa Angola.

Wakati akifunga mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Angola Joao Lourenco amesema majadiliano katika mkutano huo yalionyesha nia ya pamoja ya kuzidisha mazungumzo na kusukuma mbele ushirikiano wa kivitendo kati ya mabara hayo mawili.

Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema mpango wa Global Gateway wa EU, ambao umehamasisha uwekezaji wenye thamani ya euro zaidi ya bilioni 120 (dola za Marekani bilioni 138.8 hivi) kwa Afrika tangu kuzinduliwa kwake miaka mitatu iliyopita, unalenga kuunga mkono utoaji wa nafasi za ajira kwa watu wenyeji, maendeleo ya mnyororo wa thamani, na viwanda vya kimkakati ikiwa ni pamoja na usindikaji wa malighafi, uzalishaji wa dawa, na miunganisho ya nishati ya kikanda.

Taarifa ya pamoja ya mkutano huo imesema, pande zote mbili zimesisitiza kuunga mkono ushirikiano wa pande nyingi, utatuzi wa amani wa migogoro, na kuimarisha ushirikiano katika kupambana na ugaidi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, nishati ya kijani, mageuzi ya kidijitali, kilimo, na mifumo ya afya.

Pia wameahidi kuongeza uwekezaji, kuunga mkono maendeleo ya viwanda vya Afrika, kuimarisha utandawazi wa kikanda, na kupitisha sera ya uhamiaji yenye uwiano, ambayo inapanua njia ya halali wakati huohuo ikikabiliana na uhamiaji usio wa halali.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa, mfumo wa kudumu wa ufuatiliaji utaanzishwa ili kufuatilia utekelezaji wa ahadi za mkutano huo. Imeeleza kwamba mkutano ujao wa AU na EU utafanyika Brussels.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha