Lugha Nyingine
China yamkosoa vikali waziri mkuu wa Japan kwa kusisitiza “Mkataba wa Amani wa San Francisco” ambao ni haramu
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imemkosoa vikali Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi kwa kusisitiza "Mkataba wa Amani wa San Francisco" ambao ni haramu na batili huku akipuuza kwa makusudi nyaraka zinazofafanua majukumu ya Japan baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Alhamisi mjini Beijing, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun amesema Takaichi alichagua kukwepa Azimio la Cairo na Tangazo la Potsdam – ambayo yote mawili yanatambuliwa kuwa na nguvu kamili chini ya sheria ya kimataifa na kuthibitishwa tena kwenye nyaraka za pande mbili ikiwa ni pamoja na Taarifa ya Pamoja kati ya China na Japan ya 1972 na Mkataba wa Amani na Urafiki kati ya China na Japan - huku akirejelea "Mkataba wa Amani wa San Francisco" ambao ni haramu na batili.
Guo amesisitiza kuwa hii inaonyesha kwamba Takaichi bado anakaidi kujirekebisha, na kuendelea kuharibu msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Japan ulioanzishwa na nyaraka nne za kisiasa za pande mbili, kupuuza mamlaka ya Umoja wa Mataifa, na kupinga waziwazi utaratibu wa kimataifa wa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kanuni za msingi za sheria ya kimataifa.
Ameongeza kuwa kauli zake hata zimejaribu kuchochea "nadharia ya hadhi isiyojulikana ya Taiwan."
Akiita mbinu hiyo kosa juu ya kosa, Guo amesema China inapinga vikali na kuhimiza jumuiya ya kimataifa kuendelea kuwa na tahadhari ya juu.
“China kwa mara nyingine inatoa wito kwa Japan kujitafakari na kujirekebisha kwa makini, kufuta kauli hizo za kimakosa, na kuonyesha ahadi zake kwa China na wajibu wake kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa kupitia hatua madhubuti" amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



