Tanzania Zanzibar na China zaimarisha ushirikiano wa afya ili kupambana na magonjwa

(CRI Online) Novemba 28, 2025

(Picha/CRI)

(Picha/CRI)

Wizara ya Afya ya Tanzania Zanzibar imesisitiza dhamira yake ya kudumisha ushirikiano na China ili kuimarisha huduma za afya katika visiwa vyote vya Zanzibar, hasa katika mapambano dhidi ya kichocho na magonjwa mengine.

Mkurugenzi wa Wizara hiyo, Dkt. Amour Suleiman Mohamed, amesema hayo kwenye mkutano na ujumbe kutoka Taasisi ya Afya ya Umma ya Mkoa wa Jiangsu, ambayo imekuwa ikiunga mkono programu za kudhibiti magonjwa visiwani Zanzibar kwa muda mrefu.

Amebainisha kuwa ushirikiano huo wa muda mrefu unajumuisha kupelekwa kwa madaktari bingwa kila mwaka katika hospitali za visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na msaada mkubwa katika juhudi za kutokomeza kichocho hasa Pemba, ambapo kiwango cha maambukizi sasa kimeshuka hadi chini ya asilimia moja.

Amesema, tangu wakati huo timu ya wataalamu wa China imehamisha shughuli zake hadi Unguja, ikifanya kazi kwa karibu na kitengo cha Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa (NTD) cha Wizara hiyo na kuwezesha programu za kubadilishana wataalamu wa afya kutoka pande zote mbili.

Dkt. Amour ameongeza kuwa Taasisi ya Mkoa wa Jiangsu pia inashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Zanzibar (ZAHRI) katika kujenga uwezo wa kiufundi, kufanya utafiti wa pamoja na kuunga mkono mipango ya afya inayotegemea utafiti.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Deng Jie)

Picha