Lugha Nyingine
Wataalamu wa China wachochea kilimo jumuishi, wakibadilisha maisha ya vijijini nchini Ethiopia

Picha hii iliyopigwa Novemba 26, 2025 katika Kijiji cha Godino Jitu, Ethiopia, ikionyesha trekta lililotolewa na timu ya wataalamu wa kilimo wa China. (Xinhua/Liu Fangqiang)
ADDIS ABABA - Asnakech Sitotaw anakumbushia siku ngumu ambapo shamba lake dogo katika kijiji cha mbali katikati mwa Ethiopia halikuwa likizalisha chakula cha kutosha. Leo, kutokana na uungaji mkono wa wataalamu wa kilimo wa China, mama huyo mseja wa watoto watano anasherehekea maisha yaliyobadilika.
Makazi ya Sitotaw katika Kijiji cha Godino Jitu, Mkoa wa Oromia, yamekuwa mfano mzuri wa tija na matumaini, yakiwa na bustani ya yadi ya nyuma ya nyumba inayostawi, bwawa jipya la samaki, banda la kuku, na mengineyo.
"Siku za nyuma, mavuno yetu yalikuwa machache, hasa kutokana na ukosefu wa mbegu zenye mavuno mengi na ujuzi wa mbinu za kisasa za kilimo," amesema Sitotaw, akiwasifu wataalamu wa China kwa kumpa ujuzi ambao umebadilisha mbinu yake ya kilimo.
Mwezi Mei 2024, kundi la nne la wataalamu wa kilimo wa China nchini Ethiopia lilizindua mradi wa kivumbuzi wa miaka mitatu wa kupunguza umaskini katika kijiji hicho, kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo ya Ethiopia na serikali ya mtaa. Wataalamu hao walimpa Sitotaw na wanajamii wengine mbegu bora, pembejeo muhimu za kilimo, na mafunzo ya vitendo.
"Tunapanga kutumia uzoefu wa China katika kupunguza umaskini kwenye kijiji kupitia kutumia mbegu zenye mavuno mengi, mbinu za kilimo za hali ya juu, mashine za kilimo, na umwagiliaji unaookoa maji," amesema Zhang Shihong, mkuu wa timu hiyo ya wataalamu wa kilimo wa China.
Kazi yao inahusisha ufugaji wa mifugo, kilimo cha bustani, kilimo cha mazao, uyoga unaoliwa, na mashine za kilimo, ikilenga kuimarisha sekta ya kilimo na usalama wa chakula wa Ethiopia.
Abu Negash, baba wa watoto wawili, ni mnufaika mwingine katika kijiji hicho. Kwa uungaji mkono huo wa wataalamu Wachina, amejenga bwawa la samaki kwenye ua wa nyuma ya nyumba na kupokea mbegu za mazao zenye mavuno mengi.
"Shukrani kwa uungaji mkono wao, ikiwa ni pamoja na pembejeo na mafunzo bora ya kilimo, tumeongeza uzalishaji wetu kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita," Negash amesema.
Pia anatarajia mabanda mapya ya kuku kutoka kwa wataalamu hao wa China, ambayo yaitaimarisha mfumo wake jumuishi wa kilimo unaochanganya kuku, samaki, na mazao kwa ajili ya kujenga kipato na maisha himilivu.
Baada ya miezi sita, mabadiliko yanaonekana.
Assefa Gudissa, naibu msimamizi wa Godino Jitu, amebainisha "matokeo makubwa" ya kazi hiyo ya wataalamu katika eneo hilo. Mavuno ya ngano, kwa mfano, yameongezeka kutoka tani 4.2 hadi karibu tani 7 kwa hekta mwaka huu, mafanikio aliyoyasifia kuwa yanatokana na juhudi za wataalamu hao za kujenga uwezo na utoaji wa pembejeo za kilimo na nyenzo muhimu za kilimo.
Gudissa pia amezungumzia mchango wao zaidi ya kilimo. Amesema, kwa kushirikiana na kampuni ya kutoa huduma za mawasiliano ya nchini humo, wataalamu hao wamesaidia kujenga mnara mpya wa mawimbi ya mawasiliano kijijini hapo, kuboresha muunganisho na kuunga mkono maendeleo mapana ya jamii.

Abu Negash (kushoto), na mahindi yaliyovunwa punde, akiwa kwenye picha ya pamoja na mwanawe na mtaalamu wa kilimo wa China kwenye Kijiji cha Godino Jitu katika Mkoa wa Oromia, Ethiopia, Novemba 26, 2025. (Xinhua/Liu Fangqiang)

Zhang Shihong (kulia), mkuu wa timu ya wataalamu wa kilimo wa China, akizungumza na wenyeji kwenye Kijiji cha Godino Jitu katika Mkoa wa Oromia, Ethiopia, Novemba 26, 2025. (Xinhua/Liu Fangqiang)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



