Ethiopia yazindua mkakati wa miaka mitano kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa kidijitali

(CRI Online) Desemba 01, 2025

Serikali ya Ethiopia imezindua Mkakati wa Kidijitali wa Ethiopia wa 2030, unaolenga kukuza mafungamano ya teknolojia katika sekta zote za kiuchumi na kuufanya uchumi wa nchi hiyo kuwa wa kidijitali.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imetoa taarifa kuwa Baraza la Mawaziri la Ethiopia juzi Jumamosi liliidhinisha mkakati huo wa kitaifa wa mageuzi ya kidijitali wa miaka mitano ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za umma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumapili, mkakati huo unalenga kuimarisha uwezo wa kiteknolojia, kupanua miundombinu muhimu, na kutoa fursa mpya za kijamii na kiuchumi kwa raia, hasa vijana ambao idadi yao inaongezeka kwa kasi nchini humo.

"Kufuatia kukamilika kwa mafanikio kwa Mkakati wa Kidijitali wa Ethiopia wa 2025, ambao ulijikita katika uvumbuzi unaoendeshwa na teknolojia na ujenzi wa mambo ya kisasa, sasa tumezindua Mkakati wa Kidijitali wa Ethiopia wa 2030, ambao utaimarisha utoaji wa huduma kupitia matumizi makubwa zaidi ya mashine na mifumo ya otomesheni" amesema waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha