Lugha Nyingine
Mkuu wa MONUSCO atembelea Goma wakati mfumo wa kusimamia usimamishaji mapigano ukipata maendeleo
Kaimu Mkuu wa Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) Vivian van der Perre, amewasili Goma jana Alhamisi, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa mfumo wa kufuatilia na kuhakiki makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya serikali ya DRC na waasi wa kundi la M23.
Helikopta iliyokuwa imembeba van der Perre ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma, ambao umefungwa tangu mji huo wa mashariki ulipoangukia mikononi mwa M23 mwezi Januari 2025 na kusababisha ugumu wa utoaji misaada ya kibinadamu na usafiri wa kidiplomasia katika eneo hilo lililoathiriwa na migogoro.
“Natumai huu ni mwanzo wa kuanza kufunguliwa tena hatua kwa hatua kwa uwanja wa ndege Goma kwa manufaa ya watu,” van der Perre amewaambia waandishi wa habari punde baada ya kuwasili.
Pia amesema, ujumbe wa upelelezi utatumwa katika siku zijazo katika mji wa Uvira, Jimbo la Kivu Kusini ili kutathmini hali ya usalama na kiufundi kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huo wa usimamizi katika eneo hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



