Lugha Nyingine
Washiriki kwenye Mkutano wa Viongozi wa Nishati ya Nyuklia waahidi nishati ya nyuklia salama na nafuu
![]() |
| Picha hii iliyopigwa Machi 10, 2026 ikionyesha mjadala wa jopo kwenye Mkutano wa pili wa Viongozi wa Nishati ya Nyuklia mjini Paris, Ufaransa. (Xinhua/Wu Huiwo) |
PARIS – Nchi zaidi ya 30, zikiwemo Ufaransa, China, Canada na Japan, zimeahidi kusukuma mbele uvumbuzi wa nyuklia na kuunga mkono maendeleo na ujengaji uwezo wa nyuklia kwenye Mkutano wa pili wa Viongozi wa Nishati ya Nyuklia, uliomalizika Jumanne wiki hii jijini Paris.
Wakuu wa nchi, viongozi wa serikali na wawakilishi waandamizi kutoka nchi zaidi ya 30, vilevile mashirika husika ya kimataifa, walihudhuria mkutano huo na kutoa taarifa ya pamoja yenye kichwa "Nishati ya nyuklia salama na nafuu kwa wote."
Kwenye taarifa hiyo, washiriki wameahidi kuendelea kusukuma mbele uvumbuzi wa kiteknolojia, kuboresha zaidi ufanisi wa uendeshaji, usalama na uwezekano wa kiuchumi wa mitambo ya nyuklia, kuimarisha uhimilivu na usalama wa sekta ya nishati ya nyuklia duniani na minyororo yake ya usambazaji, na kutoa michango chanya kwa maendeleo ya kiviwanda, ushirikishwaji wa wadau na juhudi za kujenga uwezo kwa nchi husika, hasa katika nchi ambazo ni mpya au zinazotafuta namna ya kuendeleza nishati ya nyuklia.
Wakati huo huo, ushirikiano wa kimataifa wa nyuklia wa China umevutia ufuatiliaji na mapongezi mengi kutoka kwa washiriki kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Ufaransa na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Tangu miaka ya 1980, kampuni ya umeme ya Ufaransa EDF imedumisha ushirikiano na China katika sekta ya nyuklia. Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti na Ofisa mtendaji mkuu wa EDF Bernard Fontana amesema kwamba kupunguza gesi chafu katika maendeleo ya uchumi, kupanda kwa gharama za nishati, na upanuzi wa vituo vya data na AI vinaifanya nishati ya nyuklia kuwa moja ya suluhu muhimu.
Akirejelea ukamilishaji haraka wa miradi na udhibiti wa gharama, amebainisha kuwa washirika wa China wamechangia uzoefu wao wa mafanikio wakati huohuo akitoa shukrani zake kwa upande wa China kwa juhudi zake katika kusukuma mbele ushirikiano uliopo.
Pang Songtao, Mkuu wa Shirika Kuu la Nishati ya Nyuklia la China (CGNPC), pia amesema maendeleo ya CGNPC yalianza na ushirikiano kati ya China na Ufaransa kwenye Mtambo wa Nishati ya Nyuklia wa Ghuba ya Daya, ikifuatiwa na ujenzi wa pamoja wa Mtambo wa Nishati ya Nyuklia wa Taishan na Ufaransa.
“CGNPC itaendelea kupanua ushirikiano wake wa ng’ambo, ikijijumuisha kikamilifu katika mfumo wa ikolojia wa sekta ya nishati safi wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, na kuipa dunia kila wakati nishati salama, tulivu, ya kijani na safi,” ameongeza.
Gaspard Liyoko Mboyo, mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika ya Nishati ya Nyuklia, amesema China inasonga mbele katika nishati ya nyuklia, ambayo bara la Afrika lina mahitaji makubwa. Amesema, mazingira hayo yanajenga uwezekano wa ushirikiano kati ya Afrika na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




