Lugha Nyingine
Iran yafanya mazishi kwa askari wa meli ya kivita iliyozama, afisa mkuu wa usalama na kamanda wa kikosi cha Basij (7)
![]() |
| Watu wakihudhuria hafla ya mazishi mjini Tehran, Iran, Machi 18, 2026. (Xinhua/Shadati) |
TEHRAN - Watu wengi wamehudhuria hafla ya mazishi katika mji mkuu wa Iran, Tehran jana Jumatano kwa ajili ya askari wa meli ya kivita iliyozamishwa na Marekani vilevile maafisa wa juu wa usalama wa nchi hiyo na kamanda wa ngazi ya juu wa kijeshi waliouawa kwenye mashambulizi ya Israeli.
Machi 4, nyambizi ya Los Angeles-class ya Jeshi la Majini la Marekani USS Charlotte ilipindua na kuzamisha meli ya kivita ya Dena ya Iran katika Bahari ya Hindi, ikiua askari na wafanyakazi 104 waliokuwa ndani, na kuacha wengine 32 wakiwa wamejeruhiwa.
Iran imethibitisha Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa (SNSC) Ali Larijani na Gholam-Reza Soleimani, kamanda mkuu wa kikosi cha kujitolea cha Basij cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Kiislamu, waliuawa Jumanne wiki hii kwenye mashambulizi ya Israeli.
Wengine waliouawa kwenye shambulio hilo la Israel walikuwa mwana wa Larijani, Morteza, naibu katibu wa SNSC anayeshughulika na masuala ya usalama Alireza Bayat, vilevile walinzi wake kadhaa.
Hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa na wanafamilia wa marehemu, maafisa wa serikali ya Iran na makamanda wa kijeshi vilevile idadi kubwa ya watu kutoka sekta tofauti, ilianzia katika Uwanja maarufu wa Enghelab, ikishirikisha maandamano kuelekea sehemu moja iliyo kusini mwa Tehran ambako wahanga hupelekwa kwa ajili ya kuagwa kwa mara ya mwisho kabla ya mazishi yao.
Waombolezaji walikuwa wakipeperusha bendera ya Iran na kushikilia picha za "wahanga" wao, akiwemo Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ali Khamenei, walipokuwa wakiandamana kusindikiza miili hiyo. Pia wameahidi kutii na kumuunga mkono Kiongozi Mkuu mpya wa nchi hiyo Mojtaba Khamenei na kutamka kwa sauti kaulimbiu dhidi ya Marekani na Israel.
Pia wameapa kulipiza kisasi kwa Marekani na Israel kwa "uhalifu" wao na mauaji ya Wairani katika "uchokozi" wao dhidi ya nchi hiyo.
Februari 28, Israeli na Marekani zilianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Tehran na miji mingine kadhaa ya Iran, na kumuua Kiongozi Mkuu wa zamani Ali Khamenei, makamanda waandamizi wa jeshi, na raia. Iran ilijibu kupitia mashambulizi mfululizo ya makombora na droni dhidi ya Israeli na kambi na mali za Marekani katika nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




