Lugha Nyingine
Shirika la Data Duniani laanzishwa Beijing (2)
BEIJING - Shirika la Data Duniani (WDO) limefanya mkutano wake mkuu wa kwanza mjini Beijing, China jana Jumatatu, jambo ambalo linaashiria kuanzishwa kwake rasmi. Katika mkutano huo, wanachama walipitia na kupitisha katiba ya WDO, na kuwachagua wajumbe wake wa kwanza wa baraza na bodi ya wasimamizi.
Baraza hilo jipya lililochaguliwa lilifanya mkutano wake wa kwanza, likichagua uongozi wa shirika hilo na kupitisha mifumo na kanuni muhimu.
Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi ya WDO, kuanzishwa kwa shirika hilo kunalenga kuhimiza maendeleo ya data duniani na kuboresha mifumo ya usimamizi wake, kuwezesha ubadilishanaji na matumizi ya data kwa namna inavyozingatia sheria, iliyo salama na ya kuaminika, na kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali duniani.
Yang Jie, katibu mkuu wa shirika hilo, amesema dhamira ya shirika hilo ni kuziba pengo la data, kufungua thamani ya data, na kuchochea uchumi wa kidijitali. Amesema kwa kuhimiza ujenzi wa uwezo, kubadilishana mifumo ya udhibiti, ushirikiano wa kiteknolojia na wa kiviwanda, shirika hilo linalenga kusaidia nchi na jamii zaidi kupata, kutumia na kulinda rasilimali za data kwa ufanisi zaidi.
Amesema shirika hilo pia linatarajiwa kuongeza ufanisi wa mzunguko, uendelezaji na matumizi ya data, likilenga kubadilisha data kutoka kuwa "rasilimali" tu hadi kuwa "thamani." Wakati huo huo, kwa kuimarisha uratibu katika teknolojia ya data, kanuni na mifumo ikolojia ya viwanda, linaweza pia kusaidia ukuaji endelevu na thabiti wa uchumi wa kidijitali.
Muhammadou M.O. Kah, mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Sayansi na Teknolojia kwa Maendeleo, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Usimamizi wa Data cha Umoja wa Mataifa, amesema kwamba kuanzishwa kwa shirika hilo kutawezesha nchi kushiriki katika maamuzi ya usimamizi wa data duniani.
Likiwa ni shirika la kimataifa la kitaaluma, lisilo la kiserikali na lisilo la faida lililoanzishwa kwa hiari na taasisi pamoja na watu binafsi katika sekta ya data duniani, WDO linalenga kutoa jukwaa la ushirikiano wa data duniani lenye mwelekeo wa vitendo, linalolenga sekta husika na lilioundwa kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




