China yaelezea wasiwasi mkubwa juu ya Japan kupanga makombora ya masafa marefu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 02, 2026

BEIJING - China inaelezea wasiwasi mkubwa juu ya Japan kupanga makombora ya masafa marefu katika majimbo ya Kumamoto na Shizuoka, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amesema jana Jumatano.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, makombora hayo ya masafa marefu yenye uwezo wa kujibu mashambulizi yamewekwa rasmi katika matumizi kwa mara ya kwanza katika kambi mbili za Kikosi cha Ardhini cha Kujilinda (GSDF) nchini Japan.

"Japan, kwa kisingizio cha ulinzi na mashambulizi ya kujibu, inaendelea kupanga silaha za kushambulia, hatua inayozidi kwa kiasi kikubwa wigo wa 'kujilinda' na sera yake ya kujilinda pekee," msemaji Mao alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari, akiongeza kuwa "ubeberu mpya wa kijeshi" wa Japan unatishia amani na utulivu wa kikanda, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa macho kwa kiwango cha juu dhidi yake.

"Hatua ya Japan inakiuka kwa kiasi kikubwa nyaraka za kisheria za kimataifa kama vile Azimio la Cairo, Tangazo la Potsdam na Hati ya Kujisalimisha ya Japan, na pia inakwenda kinyume na katiba ya Japan na kanuni za ndani zilizopo," Mao amesema.

Ameongeza kuwa, hali hiyo kwa mara nyingine inaonyesha kwamba nguvu za mrengo wa kulia nchini Japan zinasukuma sera ya usalama ya nchi hiyo kuelekea mwelekeo wa kijeshi wa kushambulia na kupanuka.

"Pia nimebaini kuwa makundi na watu wengi nchini Japan wametoa upinzani wao hadharani," Mao amesema.

“Hivi karibuni, afisa wa Vikosi vya Kujilinda vya Japan (SDF) alivamia ubalozi wa China nchini Japan kinyume cha sheria akiwa na kisu,” Mao amesema, akiongeza kuwa badala ya kujitafakari kuhusu udhaifu katika usimamizi na kupoteza udhibiti wa SDF, Japan inaendelea kuchochea vitisho vya nje na kuharakisha uimarishaji wa kijeshi. "Mwelekeo huu ni hatari sana."Amesema.

"Tunaisihi Japan kutafakari kwa kina historia yake ya uchokozi wa kijeshi, kuheshimu ahadi zake katika nyanja za kijeshi na usalama, na kuchukua hatua kwa busara," msemaji huyo amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha