Lugha Nyingine
Rais wa Iran asema Wairani hawana uhasama wowote dhidi ya Wamarekani
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema watu wa Iran hawana uhasama wowote dhidi ya watu wa Marekani, akiishutumu serikali ya Marekani kupigana na Iran kama "wakala wa Israel."
Ametoa kauli hiyo katika barua aliyowaandikia watu wa Marekani wakati akielezea juu ya misimamo ya Iran kuhusu vita vinavyoendelea dhidi ya Marekani na Israeli.
"Watu wa Iran hawana uhasama wowote dhidi ya mataifa mengine, wakiwemo watu wa Marekani, Ulaya, au nchi jirani," Bw. Pezeshkian amesema, akiongeza kuwa, "hata wakati wa kukabiliana na uingiliaji na mashinikizo ya mara kwa mara ya nje katika kipindi chote cha historia yao ya kujivunia, Wairan wamekuwa wakitofautisha dhahiri kati ya serikali na watu zinaowatawala.”
Amesema kuielezea Iran kuwa ni tishio ni simulizi iliyotengenezwa na Israeli ili "kukwepesha ufuatiliaji wa kimataifa kutoka kwa uhalifu wake dhidi ya Wapalestina."
Akijibu vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump vya kufanya mashambulizi makubwa kwenye vituo vya nishati vya Iran katika siku zijazo, Bw. Pezeshkian amesema kushambulia miundombinu muhimu ya nchi hiyo ni kulenga moja kwa moja watu wa Iran, akisisitiza kwamba vitendo kama hivyo ni sawa na "uhalifu wa kivita" na vinajumuisha madhara yanayoenea zaidi ya mipaka ya Iran.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



