Lugha Nyingine
Wang Yi asema hatua za Baraza la Usalama hazipaswi kuhalalisha operesheni za kijeshi zisizoidhinishwa
BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kwamba hatua za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hazipaswi kutoa uhalali wa kisheria kwa operesheni za kijeshi zisizoidhinishwa, wala hazipaswi kuongeza mvutano au kuzidisha mgogoro.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ametoa kauli hiyo Alhamisi wakati wa mazungumzo ya simu na Kaja Kallas, Mwakilishi Mkuu wa Mambo ya Nje na Sera ya Usalama wa Kamisheni ya Ulaya.
Kallas ametoa maoni yake kuhusu hali ya Mashariki ya Kati na alipongeza juhudi za China za upatanishi wa kidiplomasia katika kupunguza mvutano, ikiwemo mpango mpya wa pamoja wa pointi tano uliotolewa na China na Pakistan wa kurejesha amani na utulivu katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati.
Kallas amesema upande wa Ulaya unaunga mkono operesheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa, ulinzi wa raia na malengo yasiyo ya kijeshi, na utafanya kila juhudi kuhakikisha kufunguliwa kwa njia za usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kwa upande wake Wang amesema kwamba katika hali ya sasa ya msukosuko wa kimataifa, ni jukumu la pamoja la China na Ulaya kuimarisha mawasiliano, na kulinda mfumo wa kimataifa unaozingatia Umoja wa Mataifa pamoja na utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria za kimataifa.
Amefafanua msimamo wa China kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, akibainisha kuwa mpango wa pointi tano uliopendekezwa na China na Pakistan unaonyesha maafikiano mapana ya kimataifa, ambavyo vipengele vyake vikuu vinajumuisha kukomesha uhasama, kuanza kwa mazungumzo ya amani mapema iwezekanavyo, kuhakikisha usalama wa malengo yasiyo ya kijeshi na njia za usafirishaji baharini, pamoja na kulinda kipaumbele cha Katiba Umoja wa Mataifa.
"Hatua za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinapaswa kujikita katika kutuliza hali na kupunguza mvutano," Wang amesema, akiongeza kuwa China inapenda kuendeleza mawasiliano na ushirikiano na upande wa Ulaya ili kuhimiza kukomeshwa mapema kwa uhasama na kurejesha amani ya kikanda.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni kuhusu uhusiano kati ya China na EU. Wang amesema kwamba maendeleo ya China yanatoa fursa kwa Ulaya, na kwamba changamoto zinazoikabili Ulaya hazitokani na China.
Naye Kallas amesema kwamba upande wa Ulaya unaitazama China kama mshirika muhimu wa ushirikiano, haukusudii kutengana na China, na unatarajia kuendeleza mazungumzo na mawasiliano kati ya pande hizo mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



