China yasema Mlango Bahari wa Hormuz utaendelea kutokuwa tulivu iwapo vita havitaisha

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2026

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema Alhamisi kwamba suala la usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ni athari ya kusambaa kutoka kwa migogoro ya sasa, akibainisha kuwa Mlango Bahari huo utaendelea kutokuwa tulivu iwapo vita havitaisha.

Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ametoa kauli hiyo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud yaliyofanyika Alhamisi.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia amemfahamisha Wang kuhusu hali mpya ya Mashariki ya Kati, akisema vita nchini Iran vimesababisha athari kubwa kwa nchi za eneo hilo na dunia kwa ujumla.

“Saudi Arabia inaweka umuhimu kwenye jukumu la China katika masuala ya kimataifa, na inathamini ushirikiano wa kimkakati wa ngazi ya juu na China,” amesema, akiongeza kuwa nchi hiyo inapenda kuimarisha mashauriano na uratibu na China kwenye majukwaa ikiwemo Umoja wa Mataifa, ili kwa pamoja kupunguza mvutano na kumaliza mgogoro huo.

Kwa upande wake Wang amesema kuwa vita vya muda mrefu nchini Iran, ambavyo vimeshadumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, vimesababisha vifo, majeruhi na hasara kubwa, na kudhoofisha usalama na utulivu wa Saudi Arabia na nchi zingine za Ghuba, jambo ambalo China imelifuatilia kwa karibu na kulielezea wasiwasi wake.

Wang amesema hivi karibuni China na Pakistan zilitoa mpango wa pamoja wa pointi tano wa kurejesha amani na utulivu katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, unaojumuisha kulinda mamlaka na usalama wa nchi za Ghuba, kusimamisha mashambulizi dhidi ya raia na malengo yasiyo ya kijeshi, na kuhakikisha usalama wa njia za usafirishaji baharini.

Wang amesema kuwa kipaumbele cha juu ni kuzingatia kukomesha kwa uhasama. Ameongeza kuwa, hatua za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinapaswa kuepuka kuongeza mvutano na hazipaswi kuhalalisha operesheni za kijeshi zisizoidhinishwa; vinginevyo, hali hiyo itasababisha matatizo ya muda mrefu, huku nchi ndogo na za kati zikiwa za kwanza kuathirika.

Wang amebainisha kuwa China inathamini juhudi za Saudi Arabia katika kuhimiza amani na kusimamisha mapigano, na inapenda kushirikiana na Saudi Arabia ili kurejesha amani ya kikanda mapema iwezekanavyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha