Lugha Nyingine
Taarifa zaidi zatolewa baada ya watoto 4 kuuawa kwenye tukio la kuchomwa kisu shuleni Uganda
KAMPALA – Jeshi la Polisi la Uganda limetoa maelezo zaidi jana Alhamisi juu ya tukio la kuchomwa kisu lililosababisha vifo vya watoto wanne katika Shule ya Mradi wa Maendeleo ya Mapema ya Watoto Wadogo ya Ggaba (Ggaba Early Childhood Development Program Program School) lililotokea katika mji mkuu, Kampala.
Kwa mujibu wa Rachael Kawala, msemaji wa Polisi wa Jiji la Kampala, mshukiwa aliyetambuliwa kwa jina la Okello Christopher Onyu yuko kizuizini baada ya kudaiwa kuwachoma kisu na kuwaua watoto hao wanne.
Kawala amewaambia waandishi wa habari kwenye eneo la tukio kwamba mshukiwa alikuwa ametembelea shule hiyo siku mbili mapema akitaka kumdahili mtoto wake. "Aliambiwa arudi leo. Inasemekana hata alilipa ada ya kudahiliwa kwa mtoto wake na baada ya hapo, alianza kuwachoma kisu watoto hao," msemaji huyo amesema.
Ameongeza kuwa miili ya watoto hao wanne waliofariki ilikuwa imepelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. "Tutamhoji ili kupata sababu ya kushambulia kituo hiki cha kulelea watoto," Kawala amesema.
Inspekta Jenerali wa Polisi Abbas Byakagaba, ambaye alitembelea eneo la tukio mapema siku hiyo, ameutaka umma kuwa na utulivu na kutoa taarifa yoyote inayohusiana na mshukiwa huyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, baada ya kutekeleza shambulio hilo, mshukiwa alikimbilia kwenye jumuiya ya makazi iliyo karibu, ambapo alikamatwa na umati wa watu wenye hasira waliojaribu kumuua kwa nguvu.
Polisi na wanajeshi walifyatua risasi hewani ili kuutawanya umati wa watu kabla ya mshukiwa kukamatwa na kuchukuliwa na lori la polisi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



