Lugha Nyingine
Trump atishia Iran kuwa inaweza "kuangamizwa" ndani ya usiku mmoja, akitaja mafuta ya Iran na tozo kwenye Mlango Bahari wa Hormuz
WASHINGTON - Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba Iran inaweza "kuangamizwa" ndani ya usiku mmoja na usiku huo "huenda" ukawa Jumanne jioni, ikiwa ni muda wa mwisho Trump alioweka kwa Iran kufikia makubaliano na kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, huku akidai kwamba mazungumzo na upande wa Iran kupitia wapatanishi juu ya makubaliano hayo "yanaendelea vizuri."
"Nchi nzima inaweza kuangamizwa ndani ya usiku mmoja, na usiku huo unaweza kuwa kesho usiku," Trump amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumatatu katika Ikulu ya White House.
"Hiki ni kipindi muhimu sana," Trump alisema kuhusu muda huo wa mwisho wa Jumanne. "Wana muda hadi kesho saa 2 (usiku)."
Trump pia amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari kwamba utawala wake una mpango wa kushambulia na kuharibu madaraja na miundombinu ya umeme kote Iran ifikapo usiku wa manane Jumanne.
"Ninamaanisha uharibifu kamili ifikapo saa 6 usiku. Na hilo linaweza kutokea ndani ya saa nne kama tungetaka. Hatutaki hilo litokee," Trump ameongeza.
Wakati huo huo, Trump amesema kwamba Iran ni "mshiriki mzuri na mwenye nia" katika mazungumzo hayo, akidai mazungumzo kupitia wapatanishi "yanaendelea vizuri."
Trump alisema mapema Jumatatu kwamba utawala wake umepitia pendekezo la kusimamisha mapigano kwa siku 45 katika vita dhidi ya Iran, akilielezea kuwa ni "hatua muhimu sana" lakini "haitoshi," huku Tehran ikisema "hakuna mtu mwenye akili timamu" angekubali pendekezo hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema Jumatatu kwamba kusimamisha mapigano kutawapa wapinzani muda wa kujipanga upya na kufanya uhalifu zaidi.
Trump pia amesema kwamba Marekani inapaswa kutoza tozo kwa meli zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, akisisitiza kwamba kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu ya kimataifa ya nishati kunapaswa kuwa sehemu ya makubaliano ya kumaliza vita.
"Vipi kuhusu kutoza tozo?" Trump amesema. "Ningependelea kufanya hivyo kuliko kuwaacha (Wairani) wanufaike nazo."
Alipoulizwa kuhusu mafuta ya Iran, Trump alipendekeza tena kwamba Marekani inaweza kuyadhibiti, akirejea mifano ya hatua za Marekani nchini Venezuela baada ya jeshi la Marekani kuvamia na kumkamata kwa nguvu Rais wa Venezuela Nicolas Maduro Januari 3.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



