Watu 7 wafariki kwenye ajali barabarani katika Jimbo la Rasi ya Mashariki, Afrika Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 07, 2026

Picha hii iliyopigwa Aprili 5, 2026 ikionyesha ajali barabarani  ya kugongana kati ya gari dogo aina ya SUV na lori,  huko Gqeberha, Rasi ya Mashariki, Afrika Kusini. (Idara ya Uchukuzi ya Jimbo la Rasi ya Mashariki/kupitia Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Aprili 5, 2026 ikionyesha ajali barabarani ya kugongana kati ya gari dogo aina ya SUV na lori, huko Gqeberha, Rasi ya Mashariki, Afrika Kusini. (Idara ya Uchukuzi ya Jimbo la Rasi ya Mashariki/kupitia Xinhua)

CAPE TOWN - Watu saba wamefariki dunia kwenye ajali ya kugongana ana kwa ana kwa magari mawili juzi Jumapili alasiri katika Jimbo la Rasi ya Mashariki la Afrika Kusini, mamlaka za serikali za jimbo hilo zimethibitisha.

Taarifa iliyotolewa Jumapili jioni na Idara ya Mawasiliano ya Jimbo la Rasi ya Mashariki inasema kuwa, ajali hiyo ilitokea majira ya saa tisa mchana kwa saa za Afrika Kusini wakati gari dogo aina ya SUV lililokuwa limebeba wanaume watatu na wanawake wanne lilipogongana ana kwa ana na lori kwenye barabara kuu ya M17 kati ya KwaZakhele na Motherwell huko Gqeberha, ambao hapo awali ulijulikana kwa jina la Port Elizabeth.

Idara hiyo ya mawasiliano ya jimbo imesema kuwa watu wote saba waliokuwa ndani ya gari hilo dogo aina ya SUV walithibitishwa kufariki dunia katika ajali hiyo, wakati huohuo dereva wa lori amenusurika na alikuwa akitibiwa hospitalini.

"Chanzo cha ajali hiyo kinaendelea kuchunguzwa," imesema idara hiyo, ikiongeza kuwa polisi wamefungua kesi ya mauaji ya bila kukusudia.

Katika taarifa yake, Xolile Nqatha, mjumbe wa kamati ya utendaji wa mawasiliano katika jimbo hilo la Rasi ya Mashariki, ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za marehemu.

"Tumehuzunishwa sana na upotevu huu mbaya wa maisha ya watu saba katika tukio moja. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia ambazo zimepoteza wapendwa wao katika mazingira ya namna hii ya kuhuzunisha," Nqatha amesema.

"Tunatoa wito kwa mara nyingine tena kwa watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu sana, kuwa na subira wakati wa kuendesha magari, na kufuata kanuni za mawasiliano barabarani, hasa wakati wa msongamano mkubwa wa magari," ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha