UN yasema mashambulizi ya droni nchini Sudan yanahatarisha raia na kupunguza mwitikio wa misaada

(CRI Online) April 07, 2026

Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yameonya Jumatatu kuwa mashambulizi yanayoendelea ya droni nchini Sudan yanaua raia, kuharibu miundombinu muhimu na kuongeza mahitaji makubwa ya kibinadamu nchini kote.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mashambulizi hayo yamezidi kulenga maeneo yenye watu wengi na vituo vya afya, na hivyo kuzuia zaidi upatikanaji wa huduma muhimu huku mgogoro huo ukikaribia mwaka wake wa tatu.

OCHA imesema katika Jimbo la White Nile, shambulio la droni katika Hospitali ya Al-Jabalain Alhamisi wiki iliyopita liliripotiwa kuua wafanyakazi 10 wa afya na kujeruhi wengine 22, na kupelekea usumbufu mkubwa kwa huduma za matibabu. Nako jimboni Blue Nile, mashambulizi ya siku ya Jumatano katika soko la kijiji cha Balila na maeneo mengine, yameripotiwa kuua raia saba.

Ofisi hiyo imesema kwamba tangu mgogoro huo uanze, Shirika la Afya Duniani limethibitisha mashambulizi zaidi ya 200 kwenye vituo vya afya, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 2,000. Imesema, katika robo ya kwanza ya mwaka huu pekee, mashambulizi 13 yalithibitishwa, na kuua watu 184 na wengine karibu 300 kujeruhiwa.

Hata hivyo, ofisi hiyo imesema kwamba licha ya changamoto zinazoongezeka, shughuli za kibinadamu zinaendelea ambapo Mfuko wa Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan umetenga karibu dola milioni 200 za Marekani kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu takriban milioni 4.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha