Lugha Nyingine
Licha ya Marekani, Israeli na Iran kukubaliana kusimamisha mapigano, utekelezaji na amani bado vyaendelea kuwa vigumu

Picha hii iliyopigwa Aprili 8, 2026 ikionyesha mandhari ya mjini, Tehran, Iran. (Xinhua/Shadati)
CAIRO - Baada ya siku takriban 40 za mapigano makali, Marekani na Iran zimefikia makubaliano jana Jumatano ya kusimamisha mapigano kwa wiki mbili, huku Israeli ikiunga mkono makubaliano hayo, hali ambayo imetoa muda mfupi lakini wa kutulia katika eneo la Mashariki ya Kati lenye misukosuko, ingawa hata hivyo ripoti za hivi punde zinaonesha kuwa utekelezaji wake na amani bado vinaendelea kuwa vigumu kufikiwa.
Makubaliano hayo ambayo yamekuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu yamefikiwa katika wakati muhimu, yakija muda mfupi kabla ya tarehe ya mwisho ya Rais wa Marekani Donald Trump kwa Iran kukubali makubaliano na kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, la sivyo "ustaarabu mzima utakufa."
Jumanne usiku, huku Dunia ikijiandaa kwa mashambulizi hayo tarajiwa ya Marekani, Trump alitangaza makubaliano ya pande mbili ya "kusimamisha mapigano," kwa wiki mbili huku Tehran ikikubali "ufunguaji kamili, wa mara moja na salama" wa Mlango Bahari wa Hormuz.
Kufuatia tangazo hilo la Trump, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran nalo lilitoa taarifa haraka kuthibitisha kusimamishwa kwa mapigano.
Hata hivyo, kwa sasa meli za mafuta zimesimamishwa kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kufuatia mashambulizi ya Israeli dhidi ya Lebanon, shirika la habari la Fars linalomilikiwa kwa sehemu na serikali ya Iran limeripoti Jumatano.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habari la Fars, baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano, Tehran iliruhusu meli mbili za mafuta kuvuka kwa usalama kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
"Katika saa za hivi punde, upitaji wa meli za mafuta kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz umesitishwa kabisa," ripoti hiyo imesema, ikiongeza kuwa hali hiyo imekuja baada ya jeshi la Israeli kuishambulia Lebanon, ambayo Tehran imesema inakiuka makubaliano hayo mapya ya kusimamisha mapigano kati ya Marekani na Iran ambayo Israeli imekubali kuyafuata.
Israeli na Marekani zimesema makubaliano hayo hayaihusu Lebanon, ingawa Pakistan, ambayo imepatanisha makubaliano hayo, na Iran zimesema yanaihusu Lebanon pia.
Huku hayo yakijili, Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amesema kwamba Washington inaufanyia kazi mpango wa amani uliorekebishwa kabla ya mazungumzo ya faragha kuanza hivi karibuni mjini Islamabad.
Leavitt amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Ikulu ya White House siku hiyo ya Jumatano kwamba "Mistari myekundu ya rais, yaani, mwisho wa urutubishaji wa uraniamu nchini Iran, haijabadilika."
Leavitt amedai kwamba nia ya Marekani kufanya mazungumzo inategemea kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu ya maji ya kupitisha nishati duniani "bila vizuizi au kuchelewa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi amesema kwamba Marekani lazima ichague kati ya kuunga mkono usimamishaji huo wa mapigano au kufuata kile alichokielezea kuwa ni "kuendeleza vita kupitia Israeli," akirejelea uendeleaji wa Israeli kuishambulia Lebanon.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social baadaye siku hiyo ya Jumatano Rais wa Marekani Donald Trump amesemakwamba meli, ndege za kivita, na wanajeshi wa Marekani vinaendelea kuwepo ndani na karibu na Iran hadi makubaliano hayo yaliyofikiwa yafuatwe kikamilifu.

Ndege wa Kwarara waingia msimu wa kuzaliana huko Shaanxi, China

Eneo la kaboni-sifuri katika Mkoa wa Hainan laonyesha vitendo vya kijani vya China

Vifaa vya kisasa vya usafi vyatoa huduma kwenye Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Boao la Asia 2026

Eneo Jipya la Xiong'an la China labadilika kuwa mji wenye nguvu hai kutoka mpango
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma