Visiwa vya Kulangyu, China na Zanzibar, Tanzania, “pacha wa kiroho” katika taswira za mwingiliano wa tamaduni mbalimbali duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 28, 2026

Moja ya majengo ya usanifu wa Magharibi, kiwani Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Moja ya majengo ya usanifu wa Magharibi, kisiwani Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Wiki mbili zilizopita nilitumia takribani siku sita katika vipindi tofauti kutembelea Kisiwa cha Gulangyu kilichoko umbali wa mita chache kutoka pwani ya mji wa Xiamen katika Mkoa wa Fujian, kusini mashariki mwa China. Pamoja na mambo mengine mengi yenye kuvutia, nilipotia miguu kisiwani humo, nikiwa ni Mtanzania ninayeishi China, na niliyepata kuitembelea Zanzibar kwa mara ya mwisho mwaka jana tu mwezi Agosti, nilijikuta kwa kiasi kikubwa nikihisi kama nimeingia tena katika Eneo la Mji Mkongwe, Zanzibar, Tanzania.

Moja ya majengo ya usanifu wa Magharibi, kisiwani Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Moja ya majengo ya usanifu wa Magharibi, kisiwani Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Usanifu wa magharibi kisiwani Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Usanifu wa magharibi kisiwani Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Kuanzia kuingia kwa usafiri wa kivuko cha majini, mandhari za majengo makongwe, mabaki ya kihistoria, usanifu wa majengo wenye kuashiria mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali duniani na vilevile mitaa myembamba yenye vichochoro kibao vya watembea kwa miguu, Gulangyu ilinipa kumbukumbu fulani za kunirudisha kwenye mitaa ya mji mkongwe, Zanzibar.

Mambo mengi sana yenye mwelekeo wa ufanano kati ya visiwa hivi: Kwanza, vikiwa vyote ni visiwa katikati ya mawimbi na sauti mwanana za baharini, vimepewa majina ya kusifiwa na walimwengu. Wakati Kisiwa cha Gulangyu hufahamika sana kwa majina ya Bustani ya Baharini na Kisiwa cha Piano, Kisiwa cha Zanzibar, hasa mji wake wa mkongwe wa kihistoria, kimepewa majina kama vile kisiwa cha marashi ya karafuu, kisiwa cha paradiso, viungo vya vyakula, mapenzi na kadhalika. Sifa zake hizi za kuakisi urembo na mvuto wa kipekee zimevifanya vyote viwili kuwa mahali pa kupendelewa kutembelewa sana na watalii.

Mandhari ya mji mkongwe, Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Mandhari ya mji mkongwe, Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Pili, vyote viwili husimama kama Maeneo ya Urithi wa Dunia wa UNESCO ambayo huhifadhi historia nyingi za muunganiko wa tamaduni za Mashariki na Magharibi, ikiwapa watembeleaji hatua ya kurudi nyuma kinyakati katikati ya mandhari zenye kupendeza sana. Vinafanana sana kwa kuwa vito vya kitamaduni vya pwani vilivyoundwa na karne nyingi za biashara ya kimataifa na kukumbana kwao na historia za uhusiano wa kale wa kati ya pande mbalimbali duniani.

Kisiwa cha Kulangyu chenye mchanganyiko wa mtindo wa usanifu wa jadi wa Kusini mwa Fujian, usanifu na mitindo ya Kitamaduni ya nchi za Magharibi na Mtindo wa Veranda kilitambuliwa rasmi na UNESCO Julai, 2017, wakati mji mkongwe, Zanzibar unaowakilisha muunganiko wa kitamaduni kati ya Afrika, eneo la nchi za Kiarabu, India, na Ulaya ulitambuliwa na shirika hilo Desemba, 2000.

Watalii wakitembelea mandhari ya mitaani katika kisiwa cha Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Watalii wakitembelea mandhari ya mitaani katika kisiwa cha Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Tatu, visiwa vyote viwili vinabeba usanifu na mpango miji unaotengeneza na kuhifadhi ipasavyo mitaa na vichochoro vyembamba ambavyo ni rafiki kwa watembea kwa miguu na haviruhusu magari kuingia, ikichochea matembezi ya kurandaranda na kushangaa katikati ya majengo ya urithi, bustani, na mandhari za baharini zilizohifadhiwa vema.

Nne, katikati ya matembezi na kurandaranda huko kwenye mitaa na vichochoro nyakati za mchana na usiku, visiwa vyote viwili hushamiri kwa biashara za vyakula vitamu na vitu mbalimbali vya kienyeji kwa ajili ya kumbukumbu. Kwa kisiwa cha Kulangyu vyakula kama tambi za shacha (shā chá miàn), miviringo ya samaki (yú wán), vyakula vya baharini, na vitafunwa vya minnan ni maarufu sana. Kwa, Zanzibar vilevile vyakula kama hivyo vya baharini lakini kipekee urojo, supu ya pweza na vitafunwa kama chapati, sambusa na maandazi ni maarufu.

Watalii wakitembelea vichochoro vya Kisiwa cha Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Watalii wakitembelea vichochoro vya Kisiwa cha Kulangyu, Xiamen, China. (People’s Daily Online)

Tano, visiwa hivi vyote viwili ni kimbilio kwa mamilioni ya watalii na kwa maana hiyo utalii, huendesha sehemu kubwa ya uchumi. Watalii, kwa mamilioni huvutwa kwenye angahewa tulivu ya buluu, mwanga angavu, fukwe zenye kupendeza, na maeneo ya kitamaduni ya visiwa hivi. Kila kimoja huibua hisia ya "bustani kando ya bahari": Kwa mfano, vilima na mazingira ya kijani ya Gulangyu huendana kwa kiasi fulani na mwambao wa kitropiki wa Zanzibar na angahewa yenye harufu nzuri.

Watalii wakitembelea vichochoro vya mji mkongwe, Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Watalii wakitembelea vichochoro vya mji mkongwe, Zanzibar, Tanzania. (People’s Daily Online)

Sita, ingawa Kisiwa cha Gulangyu kinasisitiza sana urithi wa piano na muunganiko wa tamaduni za Kichina na za nchi za Magharibi, huku Zanzibar ikiangazia zaidi milango ya Waswahili kwa dunia na njia za biashara ya viungo vya vyakula, lakini urithi wao wa pamoja wa kuwa makumbusho zinazoishi za utandawazi huvifanya visiwa hivi kuwa “mapacha wa kiroho”.

Kwa maana hiyo, watalii au wasafiri wanaotafuta mvuto wa kihistoria, ushairi wa usanifu, na maeneo bora ya visiwani au fukwe zenye utulivu na hali ya mapumziko watabaini kuwa sehemu zote hizi mbili za visiwani ni zenye kuvutia sawia, zikiunganisha mabara mbalimbali kupitia simulizi za biashara, uhimilivu, na mapatano ya kitamaduni.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha