Safari za utalii na matumizi wakati wa likizo ya Mei Mosi nchini China, vyote vyaongezeka ikilinganishwa na mwaka jana (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2026
Safari za utalii na matumizi wakati wa likizo ya Mei Mosi nchini China, vyote vyaongezeka ikilinganishwa na mwaka jana
Watalii wakitazama onyesho kwenye eneo la utalii la Mtaa wa Kale wa Hetou katika Eneo la Fengnan, Tangshan, Mkoa wa Hebei, kaskazini mwa China, Mei 5, 2026. (Picha na Liu Mancang/Xinhua)

BEIJING - Soko la kitamaduni na utalii nchini China liliendelea kuwa na ukuaji thabiti wakati wa likizo ya Mei Mosi 2026, huku safari za utalii wa ndani pamoja na matumizi vikiongezeka ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huo, kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa Alhamisi.

Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China imesema kwamba jumla ya safari milioni 325 za utalii wa ndani zilifanyika kote nchini China wakati wa kipindi cha Mei 1 hadi Mei 5, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.6 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Ikirejelea mahesabu ya kituo chake cha data, wizara hiyo imesema matumizi ya utalii wa ndani yalifikia yuan bilioni 185.49 (sawa na dola za Marekani bilioni 27.08), ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.9 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Wizara hiyo imebainisha kuwa taasisi za kitamaduni za umma kote nchini ziliandaa shughuli za kitamaduni takriban 49,400 wakati wa likizo hiyo, zikivutia watu takribani milioni 88 kufanya utalii.

Imesema, matumizi ya utamaduni na utalii wa usiku yaliendelea kuwa imara, huku maeneo ya matumizi ya utamaduni na utalii wa usiku ya ngazi ya kitaifa yakipokea watu zaidi ya milioni 80.41, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.44 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Aidha, China ilishuhudia ukuaji mkubwa katika sekta ya maonyesho ya sanaa jukwaani wakati wa likizo hiyo. Takriban Maonyesho 32,000 ya kibiashara, bila kujumuisha maonyesho katika kumbi za burudani, yalifanyika kote nchini China, yakizalisha mapato ya tiketi ya yuan bilioni 2.48, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.66 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hicho.

Takwimu hizo nzuri za likizo zimeonyesha umuhimu unaozidi kuongezeka wa sekta ya utamaduni na utalii katika muundo mpana wa uchumi wa China.

Takwimu rasmi zilizotolewa hapo awali na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China zilionesha kwamba thamani iliyoongezwa ya sekta zinazohusiana na utamaduni nchini China ilichangia asilimia 4.61 ya pato la taifa (GDP), huku sekta zinazohusiana na utalii zikichangia asilimia 4.35.

Mvuto wa China kwa utalii wa kimataifa pia umeendelea kuongezeka. Mwaka 2025, idadi ya watalii walioingia China ilizidi milioni 150, ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 17 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, huku matumizi ya watalii walioingia China yakizidi dola bilioni 130 za Marekani, ongezeko la karibu asilimia 40.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha