Lugha Nyingine
Hali mbaya ya hewa nchini Afrika Kusini yaainishwa rasmi kuwa janga la nchi (2)
CAPE TOWN - Serikali ya Afrika Kusini imeiainisha rasmi hali mbaya ya hewa inayoathiri majimbo kadha wa kadha kote nchini humo kuwa ni janga la nchi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi usiku, Wizara ya Usimamizi wa Ushirikiano wa Kitaifa (DCoG) imesema kwamba tangu Mei 4, mvua kubwa, mafuriko, radi, upepo mkali na theluji vimesababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na mvurugiko wa huduma muhimu katika majimbo ya Western Cape, Eastern Cape, Northern Cape, North West, Free State na Mpumalanga.
Baada ya mashauriano na vyombo mbalimbali vya serikali na mamlaka za usimamizi wa majanga za majimbo husika, na baada ya kutathmini ukubwa na ukali wa hali hiyo mbaya ya hewa, mkuu wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa chini ya DCoG Elias Sithole amesema, "Ninatoa taarifa kwamba ninaona tukio hili kuwa ni janga na ... kuliainisha janga hili kuwa ni janga la nchi."
Amesema kuwa uainishaji huo sasa unaweka wajibu mkuu ambao serikali ya nchi itaubebe katika kuratibu na kusimamia maafa.
Sithole ametoa wito wa kuitaka serikali kuimarisha zaidi uungaji mkono kwa mifumo ya usimamizi wa maafa ili kutekeleza mipango ya kukabiliana na hali ya dharura na kuhakikisha hatua zinawekwa ili kuwezesha vitengo vya mambo ya utawala vya serikali ya nchi kukabiliana kwa ufanisi na athari za maafa.
Amependekeza zaidi kwamba serikali kuu , za majimbo na manispaa zitekeleze "mpango wa idara mbalimbali wa kuzuia, kupunguza athari ya maafa, kutoa msaada na kurudisha hali ya kawaida" ili kukabiliana na athari za maafa, wakati huohuo ziwasilishe ripoti kuhusu hali ya kazi zinazoendelea ili kuwezesha serikali kufuatilia na kusimamia hatua za kukabiliana na maafa zinazotekelezwa na idara za serikali, manispaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na maeneo ya makazi yaliyoathiriwa.
Majimbo mbalimbali nchini humo yakiendelea na shughuli za uokoaji na usafishaji baada ya kukumbwa kwa siku kadhaa za mafuriko, kuporomoka kwa miundombinu, kufungwa kwa barabara na kukatika kwa umeme. Idara husika hazijatoa mara moja takwimu mpya za vifo na majeruhi.
Katika jimbo la Western Cape, Wilaya ya Manispaa ya Garden Route imesema katika taarifa yake ya jana Jumapili asubuhi kwamba maeneo kadhaa yanaendelea kuwa katika hali ya kutengwa, ambapo baadhi ya maeneo ya makazi bado hayana umeme.
"Katika hali hii ya sasa, watu wengi bado wametengwa katika maeneo yaliyoathiriwa," imesema. "Timu za utoaji msaada wa ubinadamu zinaendelea kusambaza vifurushi vya vyakula na blanketi kwa maeneo ya makazi yanayoathiriwa na maafa.”
Wakati huo huo, Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Kusini imeonya kwamba mvua kubwa na upepo mkali vinakadiriwa kuendelea katika sehemu za Western Cape hadi kesho Jumanne.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




