Lugha Nyingine
Tanzania yalenga ukuaji wa mauzo ya nje na viwanda kupitia sera ya ushuru-sifuri ya China (2)
DAR ES SALAAM - Tanzania inatarajia kuongezeka kwa mauzo ya nje, ukuaji wa viwanda na uundaji wa ajira kufuatia utekelezaji wa sera ya ushuru-sifuri wa China kwa nchi 53 za Afrika, maafisa wamesema Jumamosi kwenye mkutano wenye kaulimbiu ya "Ushuru-Sifuri kwa Fursa za Pamoja" uliofanyika kwa ajili ya wauzaji nje wa Tanzania, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Judith Kapinga amesema mpango huo unakuja wakati muhimu ambapo Tanzania inaimarisha nafasi yake katika biashara ya kikanda na kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi na mageuzi ya viwanda.
Kapinga amesema China inaendelea kuwa mmoja ya washirika wa kimkakati zaidi wa Tanzania katika biashara na uwekezaji, huku ushirikiano wa pande mbili ukihusisha miundombinu, viwanda, kilimo, madini na utalii.
"Fursa hii ni muhimu kwa wajasiriamali wa Tanzania, na tunaishukuru sana China kwa kufungua mlango wa biashara," waziri huyo amesema.
Amesema serikali ya Tanzania itaimarisha uratibu kati ya taasisi mbalimbali, kurahisisha taratibu za biashara na kutumia mifumo inayoendeshwa na teknolojia ili kuwaunga mkono wauzaji nje wanaolenga soko la China.
Waziri huyo ametoa wito kwa sekta binafsi kuboresha ubora wa bidhaa na kuwekeza katika kuongeza thamani, uvumbuzi na ujengaji wa chapa ili kuongeza uwezo wa ushindani katika masoko ya China na ya kimataifa.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema sera hiyo ya ushuru-sifuri itaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa ushindani wa mauzo ya nje ya Tanzania katika soko la China kwa kuondoa ushuru kwa bidhaa kama vile ufuta, korosho na mazao mengine ya kilimo.
Ameongeza kuwa mpango huo pia utaunga mkono ukuaji wa viwanda nchini Tanzania kwa kuhimiza usindikaji wa mazao ya kilimo, usafirishaji wa mnyororo baridi na ukuzaji wa viwanda vya uzalishaji. Amesema, sera hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wakulima, biashara ndogo ndogo na wafanyakazi wanaohusika katika kilimo, usindikaji, usafirishaji na biashara.
Balozi Chen amesema biashara ya pande mbili kati ya China na Tanzania ilifikia dola bilioni 11.28 za Marekani mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 kulinganishwa na mwaka 2024, wakati huohuo biashara hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 iliongezeka kwa asilimia 28.1 hadi kufikia dola bilioni 2.905 za Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




