Lugha Nyingine
Mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na ADF mashariki mwa DRC yasababisha vifo visivyopungua 50 vya watu
KINSHASA – Habari zilizotolewa na vyombo vya habari na makundi ya kiraia zimesema kuwa, katika wiki iliyopita vifo vya watu vimefikia zaidi ya 50 kwenye mfululizo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ripoti hizo za vyombo vya habari nchini humo zimesema, mashambulizi hayo yametokea hasa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, ambapo wapiganaji wa ADF walifanya uvamizi, utekaji nyara, uporaji na uchomaji moto katika maeneo kadhaa.
Makundi ya kiraia yamesema kuwa, kuanzia Jumapili usiku, wapiganaji hao wa ADF wamekuwa wakishambulia vijiji vya Makumo na Mabuo kwenye eneo la Mambasa katika Jimbo la Ituri, kusababisha vifo vya watu zaidi ya 15, na kuchoma nyumba. Wakazi kadhaa pia wameripotiwa kupotea baada ya hapo.
Radio Okapi, shirika linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini DRC ikinukuu habari zilizotolewa na wajumbe wa makundi ya kiraia imesema kuwa, vijiji zaidi ya 20 katika eneo la Mambasa vimekuwa vikilengwa na mashambulizi hayo ya ADF tokea mwezi Machi, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 130 katika mashambulizo hayo.
Ujumbe wa Kuleta Utulivu wa Shirika la Umoja wa Mataifa nchini DRC siku ya Ijumaa ulilaani mashambulizi hayo ya hivi karibuni dhidi ya raia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, ingawa haikutaja majina ya wahusika.
Serikali ya DRC bado haijatoa maoni rasmi kuhusu matukio hayo ya kimabavu hivi punde zaidi.
ADF, kundi lenye silaha linalohusishwa na kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Jimbo la Afrika ya Kati, awali lilianzishwa kutokana na vuguvugu la waasi wa Uganda na linafanya shughuli zake mashariki mwa DRC. Operesheni zake zinazoendelea zimekuwa zikihimiza vikosi vya DRC na Uganda kufanya pamoja operesheni za kijeshi dhidi yake tangu Novemba 2021 zenye lengo la kufuatilia na kuangamiza kundi hilo. Licha ya operesheni hizo, waangalizi wa huko wanasema ADF inaendelea kupanua shughuli zake kwenye eneo la mashariki mwa DRC.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




