Lugha Nyingine
Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Tajikistan (3)
![]() |
| Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon kwa pamoja wakihudhuria hafla ya kusaini nyaraka za ushirikiano baada ya mazungumzo yao Beijing, China, Mei 12, 2026. (Xinhua/Li Xiang) |
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo na Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing jana Jumanne.
Rais Xi ameipongeza Tajikistan kwa maadhimisho ya miaka 35 ya uhuru wa Tajikistan na mafanikio makubwa ya maendeleo ya nchi. Amesema kuwa kuungana mkono kithabiti ni sifa wazi ya uhusiano kati ya China na Tajikistan.
"Haijalishi mazingira ya nje yanavyobadilika namna gani, China na Tajikistan zitaendelea kuwa majirani wema wanaoangaliana, marafiki wazuri wanaotendeana kwa udhati na kuaminiana, na ni washirika wazuri wanaotafuta maendeleo kwa pamoja," Rais Xi amesema.
Mwaka huu, China inaanza utekelezaji wa Mpango wake wa 15 wa Miaka Mitano. Tajikistan pia inasukuma mbele Mkakati wake wa Maendeleo ya nchi kwa kipindi cha hadi mwaka 2030. Rais Xi amesema pande hizo mbili zinapaswa kufuatilia zaidi ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na kuhusisha zaidi mikakati yao ya maendeleo ili kuunga mkono kila upande kutimiza malengo yake husika ya maendeleo.
Amesema pande hizo mbili pia zinapaswa kuongeza ushirikiano wa utekelezaji wa sheria na usalama na kupambana kithabiti na nguvu tatu za ugaidi, mafarakano na siasa kali ili kudumisha kwa pamoja utulivu wa kikanda.
Rais Xi amesema China inaikaribisha Tajikistan kuwa nchi mpya iliyosaini “Mkataba wa Jumuiya ya Upatanishi ya Kimataifa (IOMed) na iko tayari kuimarisha ushirikiano chini ya Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, mfumo wa China na Asia ya Kati na mifumo mingine, ili kuhimiza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi na kufanya juhudi kwa ajili ya kujenga mfumo wa usimamizi wa Dunia ulio wa haki na usawa zaidi.
Kwa upande wake Rais Rahmon amesema, mafanikio makubwa yamepatikana katika ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, mawasiliano na uchukuzi pamoja na kilimo,miradi mikubwa inaendelea vizuri, na mawasiliano kati ya raia yameongezeka siku hadi siku, hayo yote yanaleta manufaa halisi kwa watu wa nchi zote mbili.
Amesema Taiwan ni sehemu isiyoweza kutengwa ya China, na Tajikistan inafuata kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja.
Amesema Tajikistan inatarajia kuimarisha ushirikiano wa kufuata hali halisi katika maeneo kama vile madini muhimu, teknolojia ya AI na uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, kutoa urahisi wa kutembeleana kwa watu wa pande zote mbili, kuongeza mawasiliano ya kielimu na kuhimiza maendeleo zaidi ya uhusiano wa pande mbili.
Wakati wa ziara hiyo, pande hizo mbili pia zimesaini nyaraka zaidi ya kumi za ushirikiano katika sekta za kilimo, utamaduni, elimu, maendeleo ya ujenzi wa nyumba za kuishi, ukaguzi na karantini na usimamizi wa soko.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




