Lugha Nyingine
Jukwaa la miji duniani lafunguliwa Baku Azerbaijan kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji kwa kasi (2)
![]() |
| Wawakilishi wakiwasili kwenye ukumbi wa Mkutano wa 13 wa Jukwaa la Miji Duniani (WUF 13), Baku, Azerbaijan, Mei 17, 2026. (Xinhua/Chen Junfeng) |
BAKU – Mkutano wa 13 wa Jukwaa la Miji Duniani (WUF 13) umefunguliwa rasmi jana Jumapili mjini Baku, Azerbaijan huku viongozi, watunga sera na wataalamu wa miji duniani wakikusanyika kujadili changamoto za ukuaji wa miji kwa kasi na maendeleo endelevu ya miji.
Jukwaa hilo, litakalofanyika hadi Mei 22, linatarajiwa kujikita katika makazi ya bei nafuu na himilivu, kukabiliana na tabianchi, maendeleo ya miundombinu na ukuaji jumuishi wa miji, wakati huohuo likizipa nchi jukwaa la kutoa uzoefu wa maendeleo ya miji na suluhu za kivumbuzi.
Likiwa limeandaliwa kwa pamoja na Shirika la Mpango wa Makazi ya Binadamu la Umoja wa Mataifa na serikali ya Azerbaijan, jukwaa hilo la mwaka huu litakuwa na Mkutano wa Viongozi kwa mara ya kwanza. Mkutano huo, ulioanzishwa na serikali ya Azerbaijan, utawakutanisha wakuu wa nchi na serikali, pamoja na maafisa waandamizi, kujadili vipaumbele vya kimkakati kwa mustakabali wa miji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
"Jitihada hizi kwa mara nyingine zinaonyesha kwamba makazi na maendeleo ya miji si masuala ya kiufundi pekee, bali ni masuala ya umuhimu wa kimkakati duniani ambayo yanahitaji uongozi katika ngazi ya juu," amesema mratibu wa kitaifa wa WUF13, Anar Guliyev.
Katika siku hiyo ya ufunguzi, Azerbaijan iliongoza mkutano wa mawaziri juu ya Ajenda Mpya ya Miji. Mkutano huo uliofanyika katikati ya kipindi cha utekelezaji cha miaka 20 cha ajenda hiyo, umefanya mapitio ya hatua iliyopigwa hadi sasa, kubainisha changamoto muhimu na kujadili vipaumbele vya hatua inayofuata.
WUF iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2001, hutumika kama jukwaa la ngazi ya juu kwa mazungumzo juu ya ukuaji endelevu wa miji. Mkutano wake wa kwanza ulifanyika Nairobi mwaka 2002.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




