Lugha Nyingine
Maelfu ya watu waandamana Tokyo dhidi ya msukumo wa serikali ya Takaichi wa kurekebisha katiba ya kutetea amani (4)
![]() |
| Mwanamke aliyeshikilia bango lenye kaulimbiu akishiriki kwenye maandamano mbele ya Jengo la Bunge la Taifa la Japan, Tokyo, Japan, Mei 19, 2026. (Xinhua/Jia Haocheng) |
TOKYO - Maelfu ya waandamanaji walikusanyika mbele ya Jengo la Bunge la Taifa la Japan mjini Tokyo Jumanne jioni wiki hii kupinga majaribio ya serikali ya kudhoofisha katiba ya kutetea amani ya nchi hiyo kupitia marekebisho ya katiba na sera za upanuzi wa nguvu za kijeshi.
Kwa mujibu wa waandaaji, watu takriban 10,000 walihudhuria maandamano hayo, wakipaza sauti kupinga vikali utawala wa Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi na mipango yake ya hivi karibuni ya usalama na ulinzi.
Waandamanaji walikuwa wameshikilia mabango yaliyosomeka "Simamisha marekebisho ya katiba na upanuzi wa nguvu za kijeshi" na "Usiharibu Kifungu cha 9," huku wakitamka kauli mbiu kama vile "Simamisha kuweka makombora" na "Takaichi lazima ajiuzulu."
Yuki Hoshino, mshiriki kwenye maandamano hayo, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba watu hawataki marekebisho ya katiba, na kwamba serikali ya Takaichi inasukuma ajenda bila ridhaa ya kutosha ya umma.
Muandamanaji mwingine, Ryosuke Tanji, amesema Japan haipaswi kamwe kurudia tena majanga ya vita.
Hiroshi Onishi, profesa mstaafu katika Chuo Kikuu cha Keio, ameliambia Xinhua kwenye maandamano hayo kwamba ujengaji wa jeshi wa hivi karibuni wa serikali unapingana na kanuni za amani zilizoainishwa katika katiba ya Japan na unapaswa kusimamishwa.
Vyombo vya habari vya Japan viliripoti Jumatatu wiki hii kwamba Chama tawala cha Liberal Democratic kilikuwa kimeandaa mapendekezo ya kurekebisha nyaraka tatu muhimu za usalama wa taifa wa nchi hiyo. Mapendekezo hayo yanaripotiwa kutaka kuimarisha mifumo ya ulinzi wa anga ya Japan na uwezo endelevu wa mapigano, vilevile kuwekwa mapema kwa manowari zinazoendeshwa na mifumo ya hali ya juu ya kuziendesha na iliyoundwa kubeba makombora ya masafa marefu ili kuimarisha kile kinachoitwa "uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya kujihami" wa Japan.
Katiba ya sasa ya Japan, ambayo ilianza kutumika mwaka 1947, ina Kifungu maarufu cha 9, ambapo nchi hiyo inakataa vita kama haki huru ya taifa na tishio au matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro ya kimataifa. Kifungu hicho pia kinasema kwamba Japan haitadumisha uwezo wa kivita, na kusababisha katiba hiyo kujulikana sana kwa jina la "katiba ya kutetea amani."
Takaichi na vikundi vingine vya mrengo wa kulia nchini Japan kwa muda mrefu vimekuwa vikitetea marekebisho ya Kifungu hicho cha 9. Waziri mkuu huyo ameelezea mara kwa mara kuunga mkono marekebisho ya katiba mwaka huu, ikisababisha wasiwasi na upingaji unaozidi kuongezeka miongoni mwa umma wa Japan na sekta mbalimbali za jamii.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




