Lugha Nyingine
Maonyesho ya Kimataifa ya Mambo ya Utamaduni ya China yafunguliwa Shenzhen
SHENZHEN - Maonyesho ya 22 ya Kimataifa ya Mambo ya Utamaduni ya China yameanza rasmi jana Alhamisi katika mji wa kisasa wa Shenzhen, ulioko Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China.
Maonyesho hayo ya siku tano, ambayo yataonesha maendeleo ya sekta ya kitamaduni, yamevutia waonyeshaji 6,312 mtandaoni na nje ya mtandaoni, huku bidhaa za kitamaduni zaidi ya 120,000 zikionyeshwa.
Maonyesho hayo ya mwaka huu, kwa mara ya kwanza, yameanzisha eneo maalum la maonyesho kwa nchi na maeneo ya APEC, likionyesha mafanikio ya eneo la Asia-Pasifiki katika utalii wa kitamaduni. Bidhaa maalum za eneo hilo, bidhaa bunifu za kitamaduni zilizochochewa na urithi wa utamaduni usioshikika, na vyakula vitamu vya kikanda pia vinaonyeshwa.
Mji wa Shenzhen utakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 33 wa Viongozi wa Uchumi wa APEC mwezi Novemba mwaka huu.
Eneo lingine jipya la maonyesho lililoanzishwa linajikita katika biashara ya mtandaoni ya kuvuka mipaka. Linaleta pamoja kampuni kadhaa husika kwa lengo la kuwezesha biashara ya kuvuka mpaka katika sekta ya utamaduni na kutoa njia kwa bidhaa za kitamaduni kufikia masoko ya kimataifa.
Kwa jumla, kumbi nane za maonyesho zimeandaliwa ndani ya Kituo cha Maonyesho na Mikutano cha Shenzhen World, ukiwemo ule unaoonyesha uvumbuzi wa sekta ya utamaduni katika Eneo Kuu la Ghuba ya Guangdong-Hong Kong-Macao.
Maonyesho hayo yaliyoanzishwa mwaka 2004, yamekuwa shughuli ongozi ya kitamaduni nchini China na jukwaa muhimu la kusaidia utamaduni wa China katika kwenda duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




