Lugha Nyingine
Marais wa China na Serbia wasifu urafiki imara ulio kama wa chuma, watafuta ushirikiano mpana katika sekta mbalimbali (6)
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Serbia Aleksandar Vucic wamefanya mazungumzo mjini Beijing jana Jumatatu, wakisifu urafiki imara ulio kama wa chuma kati ya nchi hizo mbili na kuahidi kuongeza ushirikiano unaohusu kuanzia mawasiliano na uchukuzi na maeneo yanayoibukia, hadi mawasiliano kati ya watu.
Vucic yuko katika ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini China kuanzia Mei 24 hadi 28. Hapo awali alisafiri kuja China mara kadhaa kwa kushiriki kwenye shughuli za kimataifa.
Xi amesema pande hizo mbili zimefungua kwa pamoja ukurasa mpya wa kujenga jumuiya ya China na Serbia yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya tangu ziara yake ya kiserikali nchini Serbia mwaka 2024, hali ambayo imenufaisha watu wa pande zote mbili na kuweka mfano wa uhusiano kati ya nchi na nchi.
Xi amesisitiza kwamba urafiki imara kati ya China na Serbia ni wa kipekee, unaotokana na mantiki kubwa ya kihistoria na msingi imara wa kufuata hali halisi ya sasa, na amesema pande hizo mbili zinapaswa kuendelea kuungana mkono kwa uthabiti.
"Mazingira ya kimataifa yanayobadilika-badilika na yenye misukosuko yanahitaji uratibu na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya China na Serbia katika masuala ya kimataifa," Xi amesema, na kuongeza kuwa, nchi hizo mbili zinapaswa kutekeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, na kujitahidi kusukuma mbele kwa uthabiti ujenzi wa dunia yenye nchi nyingi iliyo ya usawa na utaratibu na utandawazi wa uchumi wa dunia wenye manufaa na jumuishi kwa wote, pamoja na ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Katika ziara hiyo ya Vucic, Xi amemtunuku Nishani ya Urafiki, ambayo ni nishani ya heshima ya juu zaidi inayotolewa na Jamhuri ya Watu wa China kwa raia wa kigeni.
"Nishani hii si tu ni utambuzi wa juu wa mchango aliotoa Rais Vucic kwa ajili ya urafiki kati ya China na Serbia, bali pia inabeba matarajio ya dhati ya watu wa pande mbili kwa kujenga jumuiya ya China na Serbia yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya," Xi amesisitiza.
Vucic amesema, huu ni wakati mmoja muhimu zaidi maishani mwake, na nishani hiyo si tu ni heshima kubwa kwake mwenyewe, bali pia ni utambuzi kwa Serbia iliyotafuta mamlaka ya nchi, uhuru na maendeleo.
Akisema kuwa China siku zote inaheshimu nchi ndogo, kusimama pamoja na watu wa Serbia katika nyakati ngumu, na kusaidia Serbia kupata maendeleo, Vucic amesema Serbia haitasahau kamwe uungaji mkono na msaada wa China, na ataendelea kujitolea kwa ajili ya urafiki kati ya Serbia na China na kushirikiana na China katika kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya Serbia na China yenye mustakabali wa pamoja.
Kabla ya mazungumzo, Xi na mkewe Peng Liyuan walifanya hafla ya kuwakaribisha Vucic na mkewe Tamara Vucic kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing. Xi na Peng pia walifanya dhifa ya kuwakaribisha jioni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




