Idadi ya visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola nchini DRC yazidi 1,000

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 29, 2026
Idadi ya visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola nchini DRC yazidi 1,000
Wafanyakazi wakisafirisha vifaa vya kuzuia na kudhibiti maambukizo, Bunia, Jimbo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mei 28, 2026.(Xinhua)

KINSHASA - Idadi ya visa vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imezidi 1,000 wakati ambapo mlipuko huo wa hivi punde ukiendelea kuenea katika majimbo ya mashariki, kwa mujibu wa ripoti ya hali iliyotolewa Jumatano wiki hii na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

Ripoti hiyo, inayotokana na takwimu zilizokusanywa hadi kufikia Jumanne wiki hii, imeweka idadi ya jumla ya visa vinavyoshukiwa kuwa 1,077. Nchi hiyo imerekodi visa 121 vilivyothibitishwa na vifo 238 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola tangu mlipuko huo ulipotangazwa tarehe 15 Mei.

Mlipuko huo umeathiri kanda 13 za kiafya katika majimbo ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini, na Kivu Kusini, ripoti hiyo imesema, huku Ituri ikibaki kuwa jimbo lililoathiriwa zaidi.

Mlipuko huo wa sasa ni janga la 17 la Ebola nchini humo. Vipimo vya maabara vimetambua aina ya virusi vya Bundibugyo, aina nadra ya Ebola.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Mei 17 lililitangaza janga hilo kuwa dharura ya kiafya ya umma inayohitaji umakini na ufuatiliaji wa kimataifa, na Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vililitangaza baadaye kuwa dharura ya usalama wa afya ya umma ya bara.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha