Lugha Nyingine
Timu ya madaktari Wachina yaleta huduma ya afya bila malipo kwa jamii ya Zanzibar, Tanzania (2)
![]() |
| Daktari Mchina akitoa vipindi vya elimu ya afya kwa mtoto wenyeji, Zanzibar, Tanzania, Mei 30, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman) |
ZANZIBAR - Asubuhi ya Jumamosi yenye mwanga angavu huko Kombeni, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar, Tanzania, mfanyakazi wa ulinzi mwenye umri wa miaka 71 Amin Maulid Juma alitoka kwenye Kliniki ya Sinai akiwa na hisia mpya ya unafuu na shukrani.
Kwa wiki kadhaa, alikuwa amevumilia usiku mfululizo wa kukosa usingizi kutokana na maumivu ya tumbo yasiyokoma. Lakini baada ya dakika 45 tu chini ya uangalizi wa madaktari kutoka kundi la 35 la timu ya madaktari ya China visiwani Zanzibar, hali yake iliboreka sana.
"Nimekuwa na usiku mfululizo wa kukosa usingizi kwa muda mrefu sasa, lakini leo najihisi vizuri zaidi baada ya madaktari Wachina kunitibu bila malipo," Juma amesema, akiwa ameshika pakiti za dawa alizoandikiwa na daktari.
Juma ni miongoni mwa wakazi wenyeji karibu 200 waliopokea huduma za matibabu bila malipo wakati wa kliniki ya siku moja iliyoandaliwa na timu hiyo ya madaktari Wachina kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar katika Kliniki ya Sinai. Kliniki hiyo ni sehemu ya mpango wa "Timu 100 za Madaktari katika Vijiji 1,000" wa China na iliambatana na sherehe za kuadhimisha Siku ya Watoto Duniani.
Kliniki hiyo iliwaleta pamoja madaktari bingwa Wachina katika tiba za ndani ya mwili, kama vile magonjwa ya wanawake, utunzaji wa masikio, pua na koo, upasuaji wa mdomo na uso, na dawa za jadi za Kichina. Mbali na mashauriano na matibabu, timu hiyo ilitoa vipindi vya elimu ya afya na kusambaza dawa za bila malipo kwa wagonjwa.
Kwa wakazi wengi wa Kombeni, upatikanaji wa huduma maalum za afya bado ni mdogo. Kuwasili kwa timu hiyo ya madaktari Wachina kulitoa fursa adimu ya kupata shauri kutoka wataalamu wenye uzoefu bila gharama yoyote.
Matatizo yaliyotibiwa zaidi wakati wa kliniki hiyo ni pamoja na magonjwa ya kisukari, matatizo ya macho, magonjwa sugu, na magonjwa ya kitropiki kama vile ukurutu na magonjwa mengine ya ngozi. Wagonjwa walipokea mashauriano ya ana kwa ana, dawa, na ushauri kuhusu kudhibiti hali zao.
Kliniki hiyo pia ilileta mguso mkubwa wa kibinadamu, hasa kwa watoto. Ili kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watoto, wajumbe wa timu ya madaktari Wachina walitumia pesa zao kununua zawadi kwa wagonjwa wadogo na watoto katika jamii.
Murshid Mustafa mwenye umri wa miaka saba kutoka Shule ya Watoto ya Great Future hakuweza kuzuia msisimko wake alipoonyesha kwa fahari zawadi zake.
"Nina furaha sana, na ninawashukuru madaktari Wachina kwa mchango wao wa ukarimu. Wachina watabaki kuwa marafiki zetu daima," amesema.
Bao Zengtao, kiongozi wa timu hiyo ya madaktari Wachina, amesema kliniki hiyo inaonyesha dhamira inayoendelea ya timu hiyo katika kuhudumia jamii za wenyeji.
Ameongeza kuwa shughuli za namna hiyo si tu kuhusu kutibu magonjwa bali pia ni kuhusu kujenga hali ya kuaminiana na kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania.
Usaidizi wa kimatibabu wa China kwa Tanzania ulianzia miaka ya 1960. Tangu wakati huo, timu za madaktari Wachina kwa mfululizo zimetumwa Tanzania Bara na Zanzibar, zikifanya kazi katika hospitali, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wenyeji, na kuendesha programu za kliniki katika jamii zisizo na huduma za kutosha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




