Lugha Nyingine
Jukwaa la teknolojia za kilimo la China na Afrika lafunguliwa nchini Kenya ili kuongeza ushirikiano wa kilimo

Picha hii iliyopigwa Juni 9, 2026 ikionyesha maonyesho kwenye Jukwaa la Ushirikiano wa Teknolojia za Kilimo na Viwanda la China na Afrika 2026 jijini Nairobi, Kenya. (Xinhua/Liu Qiong)
NAIROBI - Jukwaa la Ushirikiano wa Teknolojia za Kilimo na Viwanda la China na Afrika 2026 limefunguliwa jana Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, likiwaleta pamoja watunga sera, watafiti, na viongozi wa sekta ili kuzidisha ushirikiano wa kilimo na kuchochea maendeleo ya mambo ya kisasa ya bara hilo kupitia uvumbuzi, uhamishaji wa teknolojia, na ushirikiano wa kimkakati.
Jukwaa hilo la ngazi ya juu limevutia wajumbe zaidi ya 100 ambao wamejadili fursa za kupanua ushirikiano kati ya China na Afrika katika teknolojia za kilimo, uvumbuzi, biashara, na uwekezaji.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi wa China nchini Kenya Guo Haiyan amesema kwamba kadri China na Afrika zinavyoendelea kuimarisha ushirikiano chini ya mfumo wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, maendeleo ya kilimo cha kisasa yamekuwa eneo muhimu kwa ushirikiano wenye kunufaishana.
Ameelezea imani yake katika mustakabali wa ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika, akibainisha kuwa kwa kuchanganya rasilimali nyingi za kilimo na idadi ya vijana ya Afrika na uzoefu wa maendeleo, teknolojia, na fursa za soko za China, pande zote mbili zinaweza kusukuma mbele maendeleo ya kilimo cha kisasa, kuimarisha usalama wa chakula, na kufikia ustawi wa pamoja.
Hamadi Boga, makamu mkuu anayehusika na utekelezaji wa mipango katika Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika, amesema kuwa Afrika inaweza kujifunza masomo muhimu kutokana na uzoefu wa maendeleo ya kilimo wa China.
Boga amebainisha kuwa kupitia ushirikiano katika utumiaji wa teknolojia, uvumbuzi, kubadilishana maarifa, na uwekezaji, China na Afrika zinaweza kufanya kazi pamoja ili kuharakisha maendeleo ya kilimo cha kisasa, kutengeneza ajira na ustawi, na kuimarisha usalama wa chakula kote barani humo.
Willy Mutai, afisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Chai ya Kenya, amebainisha kuwa jukwaa hilo litachochea juhudi za kuongeza tija ya kilimo ya Afrika kwa kushughulikia mapengo ya teknolojia na mavuno kidogo ya kilimo ambavyo huathiri usalama wa chakula wa bara hilo.
Ameongeza kuwa kupitia kubadilishana teknolojia na kuunganisha wadau wa ushirikiano, Afrika inaweza kufaidika na sekta ya kilimo ya China iliyopiga hatua kubwa.

Watu wakihudhuria Jukwaa la Ushirikiano wa Teknolojia za Kilimo na Viwanda la China na Afrika 2026 jijini Nairobi, Kenya, Juni 9, 2026. (Xinhua/Liu Qiong)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



