Vikosi vya Iran na Marekani vyapambana baharini huku Iran ikitangaza kufungwa kabisa kwa Mlango Bahari wa Hormuz

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 11, 2026

Picha hii iliyopigwa kwa simu ya mkononi ikionyesha meli za kibiashara zilizokwama kwenye maji ya Mlango Bahari wa Hormuz, karibu na Khasab, mji mdogo kaskazini mwa Oman, Mei 29, 2026. (Xinhua/Wen Xinnian)

Picha hii iliyopigwa kwa simu ya mkononi ikionyesha meli za kibiashara zilizokwama kwenye maji ya Mlango Bahari wa Hormuz, karibu na Khasab, mji mdogo kaskazini mwa Oman, Mei 29, 2026. (Xinhua/Wen Xinnian)

TEHRAN - Mapigano yamezuka mapema Alhamisi kati ya vikosi vya Iran na Marekani kwenye maji ya Ghuba na Ghuba ya Oman, huku Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, kamandi kuu ya kijeshi ya Iran, yakitangaza kufungwa kabisa kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa meli za Marekani karibu na Mlango Bahari wa Hormuz zililengwa na makombora na droni zilizorushwa na vikosi vya jeshi la Iran.

Milipuko pia ilisikika katika kaunti za Sirik na Minab na mji wa bandari wa Bandar Abbas, maeneo yote hayo yako katika jimbo la Hormozgan, na pia kwenye visiwa vya Qeshm na Hengam, huku mifumo ya ulinzi wa anga ikianzishwa kufanya kazi magharibi mwa mji mkuu Tehran na katika jimbo la kusini la Fars, shirika la habari la Mehr ambalo ni nusu rasmi nchini Iran limeripoti.

Kufuatia matukio hayo, Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya yamesema Mlango Bahari wa Hormuz umefungwa kwa aina zote za meli, ikiwemo meli za mafuta na meli za kibiashara, kutokana na matishio ya kiusalama katika njia hiyo ya maji.

Makao Makuu hayo yametaja mwendelezo wa "vitendo viovu" na mashambulizi ya Marekani mapema siku hiyo katika jimbo la Hormozgan kusini mwa Iran, yakisema meli yoyote inayojaribu kupita kwenye mlango bahari huo italengwa kwa mashambulizi.

Mwenendo wa hali hiyo umefuatia tangazo la Kamandi Kuu ya Marekani kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii wa X, ikisema vikosi vyake vimeanza kufanya "mashambulizi mengine zaidi ya kujilinda" dhidi ya maeneo kadhaa lengwa nchini Iran katika kukabiliana na kile ilichokiita "uchokozi usio na msingi na unaoendelea wa Iran."

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha