Shahidi wa Urafiki: Safari ya masomo ya Mwanafunzi Mtanzania nchini China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 12, 2026

Chuma Mohamed Muhibu, mwanafunzi Mtanzania mwenye umri wa miaka 35, kwa sasa anasoma shahada ya uzamivu (PhD) katika Sera na Vitendo vya Elimu ya Walimu (Teacher Education Policy and Practice) katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Beijing nchini China. Imepita miaka saba tangu alipofika China kwa mara ya kwanza mwaka 2019 kwa ajili ya masomo yake. Amesema kwamba, muda huo wa kuwepo China umempa fursa nyingi za kujifunza lugha ya Kichina na utamaduni wa China, na zaidi ya yote, kuweza kupata uzoefu wa kiwango cha juu katika sekta ya elimu.

Chuma amesema, sababu kubwa iliyompelekea kusoma nchini China ni ubora wa elimu inayopatikana, pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. "China nzima nafikiri kila mtu anajua namna ya kutumia teknolojia. Hata ukiangalia wanafunzi ambao tunakutana nao katika ngazi ya chini kabisa na hata kozi nyingi ambazo tunajifunza hapa, yaani teknolojia imepewa kipaumbele. Kwa fursa tunazozipata huwa tunaona kwamba hata kufundisha unaweza kutumia teknolojia na wanafunzi wakakuelewa zaidi.”

Chuma alibeba jukumu la kuwa kiongozi wa Umoja wa Wanafunzi Watanzania Wanaosoma Beijing nchini China kwa mwaka mmoja, na jambo kubwa analojivunia ni kuhakikisha Watanzania wanasherehekea Utanzania wao katika ardhi ya kimataifa hasa kupitia shughuli mbalimbali za siku za utamaduni vyuoni. "Nilikuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba Watanzania wa maeneo mbalimbali wanashiriki. Tumekuwa tukikutana na wanafunzi wa mataifa mengine, na kujadiliana vitu tofauti tofauti, katika nyanja za uchumi, elimu...Kwangu mimi hiki kilikuwa ni kitu kizuri.”

Kwa sasa Chuma anafanya tasnifu yake ya shahada ya uzamivu kuhusu ustahimilivu wa walimu wanaojiandaa kuingia katika taaluma ya ualimu (pre service teachers) akiangazia changamoto zao, kushindwa kwao kuendelea kutokana na changamoto hizo na ustahimilivu wao dhidi ya changamoto hizo hadi kupata mafanikio.

Amesema katika siku za baadaye, baada ya kurudi nyumbani, anataka kuchangia katika sekta ya elimu ya Tanzania kwa kutumia ujuzi na elimu ambayo ameipata nchini China, ili kuhakikisha sekta ya elimu nchini Tanzania inapiga hatua. Fuatilia simulizi yake kama shahidi wa urafiki kati ya Tanzania na China na utazame safari yake ya masomo nchini China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha