Lugha Nyingine
Wiki ya Utamaduni wa Burundi kufanyika Beijing (4)
![]() |
| Sehemu ya mkutano na waandishi wa habari kwenye Ubalozi wa Burundi nchini China. (Picha/Wu Qianqian) |
Balozi wa Burundi nchini China, ambaye pia ni mwakilishi wa nchi inayoshikilia uenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, Télesphore Irambona, ametangaza kwamba Ubalozi wa Burundi mjini Beijing utafanya Wiki ya Utamaduni wa Burundi ambayo ni ya kwanza kabisa kufanyika, ikihusisha shughuli mbalimbali.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi za Ubalozi wa Burundi Juni 12, Balozi Irambona alieleza kuwa mfululizo wa shughuli za Wiki hiyo ya Utamaduni wa Burundi zenye kaulimbiu isemayo "Ngoma Takatifu ya Burundi (Ingoma) Inapoimarisha Uhusiano wa Kiutamaduni kati ya China na Afrika" zitafanyika jijini Beijing kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 1 Julai, zikihusisha kwa sehemu kubwa maonyesho ya kiutamaduni, kongamano la uwekezaji, na maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Burundi.
Kwa mujibu wa Balozi huyo, Ngoma Takatifu ya Burundi (Ingoma), ambayo ni nguzo kuu ya wiki hiyo ya utamaduni, ni ala ya muziki ya jadi ya nchi hiyo inayochukua nafasi muhimu katika maisha ya kisiasa na kiutamaduni, na kihistoria mara nyingi ikitumiwa kulaki wageni mashuhuri wa kitaifa.
Katika hotuba yake, Irambona alisema kuwa mwaka 2026 ni Mwaka wa Mawasiliano ya Kiutamaduni kati ya Watu wa China na Afrika, na wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za Afrika.
"Wiki hii ya utamaduni inalenga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kirafiki kati ya Burundi na China, wakati huohuo ikiionesha dunia taswira halisi ya Burundi" alisema.
Alisisitiza kuwa mawasiliano ya kiutamaduni yanaweza kuchochea kuelewana na kuaminiana miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali, hivyo kusaidia kujenga ushirikiano wa muda mrefu.
"Burundi inathamini sana mawasiliano ya kati ya watu na inatumai kutumia fursa hii kuzidisha kuelewana na kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili na kupata ustawi wa pamoja" alisema.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Balozi Irambona amesifu sera ya China ya kutoza ushuru-sifuri (zero-tariff) kwa bidhaa kutoka nchi zote za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia nayo.
"Hili lina manufaa makubwa kwa Afrika na linasaidia kuchochea mageuzi yake ya kiuchumi. Hatua hii itakuwa kisawazishi muhimu, ikichochea kikamilifu uzalishaji wa Afrika," alisema Irambona.
Irambona pia alieleza kuwa Afrika inajishughulisha kikamilifu na uboreshaji wa usindikaji wa bidhaa na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu, kwa lengo la kufaidika vyema zaidi na sera hiyo ya China. Wakati huo huo, alieleza matumaini yake ya kuimarishwa kwa ushirikiano na mabadilishano kati ya China na Afrika katika nyanja za kupunguza umaskini, sayansi na teknolojia.
Irambona alisema kuwa upande wa Afrika unatarajia kutumia fursa ya Mwaka wa Mawasiliano ya Kitamaduni kati ya Watu wa China na Afrika kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili. Pia alitoa wito wa kujumuisha hatua mbalimbali katika mfumokazi wa muda mrefu ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya uhusiano na ushirikiano kati ya Afrika na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




