Lugha Nyingine
Misri yafungua maktaba ya urithi katika Jumba Kuu la Makumbusho la Misri

Ahmed Ghoneim (wa kwanza, kushoto), afisa mtendaji mkuu wa Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa maktaba mpya ya urithi katika GEM, Giza, Misri, Julai 6, 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)
CAIRO - Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Misri Sherif Fathy amezindua maktaba mpya ya urithi katika Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM) jana Jumatatu.
Maktaba hiyo ina vitabu na marejeleo takriban 17,000 yanayohusu elimu ya Misri, akiolojia, makumbusho, hekaya za kale, usanifu majengo, historia na urithi wa kitamaduni.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Fathy amesema maktaba hiyo itaimarisha dhamira ya kisayansi na kitamaduni ya jumba hilo la makumbusho na kuunga mkono maendeleo yake ya kuwa kitovu cha kikanda na kimataifa cha utafiti na maarifa.
Ahmed Ghoneim, afisa mtendaji mkuu wa GEM, ameuelezea ufunguzi wa maktaba hiyo kuwa ni "hatua muhimu" katika juhudi za jumba hilo la makumbusho kuwa moja ya taasisi kuu zaidi za kitamaduni na kisayansi duniani.
"Maono ya Jumba Kuu la Makumbusho la Misri hayajawahi kamwe kuwekewa kikomo katika kuhifadhi na kuonyesha hazina za Misri ya Kale pekee. Pia ni mahali ambapo urithi, sayansi, elimu na uvumbuzi hukusanyika pamoja," Ghoneim amesema.
Maktaba hiyo inahifadhi machapisho adimu yaliyohamishwa kutoka Jumba la Makumbusho la Misri katika Uwanja wa Tahrir jijini Cairo. Kivutio kikubwa kati yao ni chapisho la Kiitaliano la mwaka 1656 ambalo linafuatilia machimbuko na maendeleo ya makumbusho.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Misri Sherif Fathy (wa kwanza, kulia), akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa maktaba mpya ya urithi katika Jumba Kuu la Makumbusho la Misri (GEM), Giza, Misri, Julai 6, 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)

Mgeni mwalikwa akitembelea maktaba mpya ya urithi kabla ya hafla ya uzinduzi katika Jumba Kuu la Makumbusho la Misri, Giza, Misri, Julai 6, 2026. (Xinhua/Xin Mengchen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



