Lugha Nyingine
Jukwaa la Davos la Majira ya Joto lafungwa Dalian, umuhimu wa China waonekana katika kuhimiza kuongeza uvumbuzi
DALIAN - Jukwaa la Davos la Majira ya Joto 2026 limemalizika jana Alhamisi katika mji wa Dalian kaskazini mashariki mwa China, likisisitiza kwamba uvumbuzi ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote wa hapo kabla katika zama za kuharakisha mabadiliko ya kiteknolojia na kuongezeka kwa hali isiyo na uhakika, na China imeonesha kazi yake muhimu.
Jukwaa hilo, yaani Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Mabingwa Wapya wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), limejadili mada kuu ya "Uvumbuzi wa Kiwango Kikubwa." Mkutano huo umefanyika kuanzia Tarehe 23 hadi 25 Juni, ambapo washiriki zaidi ya 1,700 kutoka nchi na maeneo zaidi ya 90 wamejadili njia za kubadilisha uvumbuzi kuwa fursa nzuri ya kuongeza ajira, uchumi wenye nguvu zaidi na fursa mpya za kupata ongezeko la uchumi.
Katika kumbi za mkutano na mijadala mbalimbali, mada za majadiliano zimehusisha teknolojia za AI na roboti za maumbo ya binadamu, teknolojia ya kwantumu, dawa za kiviumbe, utengenezaji bidhaa kwa teknolojia ya hali ya juu na viwanda vya kijani. Sekta hizo nyingi pia ni sekta ambazo China imejitokeza kuwa mvumbuzi na mshirika muhimu zaidi katika ushirikiano wa kimataifa. Waziri Mkuu wa China Li Qiang wakati akihutubia mkutnao wa wajumbe wote wa kufunguliwa kwa jukwaa hilo siku ya Jumatano alisema kwamba kujipatia maendeleo kwa kutegemea uvumbuzi ni muhimu kwa uhimilivu wa muda mrefu wa uchumi na ongezeko tulivu na thabiti la uchumi wa China.
"Kwa maendeleo ya uchumi wa dunia, 'Fursa ya China 2.0' inamaanisha ufikiaji mpana zaidi wa teknolojia za hali ya juu na kunufaika pamoja na matokeo ya maendeleo kwa upana zaidi," waziri mkuu huyo alisema, na kuongeza kuwa ushirikiano unaofanyika kwa kutegemea uvumbuzi ni chaguo la lazima katika kushinda mtanziko wa ongezeko la uchumi wa Dunia.
Kwenye ufungaji wa mkutano, Mirek Dusek, mkurugenzi mkuu wa WEF amesema, ingawa muundo wa siasa za kijiografia unazidi kugawanyika, uvumbuzi unabaki kuhusiana na kuunganishwa kwa kina". "Kile ambacho dunia inahitaji sasa ni mfumo wa uwekezaji, mifumo ya sera na ushirikiano wa kimataifa ili kuvipangia kwa kasi na kwa kiwango kikubwa."
Pia ametangaza kwamba Jukwaa lijalo la Davos la Majira ya Joto litafanyika katika mji wa bandari wa Tianjin kaskazini mwa China mwaka 2027.
Jukwaa hilo lililoanzishwa na WEF mwaka 2007, linafanyika kila mwaka nchini China, kwa kupeana zamu kati ya miji miwili ya bandari ya Tianjin na Dalian.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma




