Lugha Nyingine
Maoni: Kutazama Ufunguaji Mlango na Ushirikiano Kupitia Rekodi Mpya ya Thamani ya Biashara ya China-Afrika Iliyozidi Yuan Trilioni 1
Usiku unapoingia katika mji wa Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, China, malori yaliyosheheni matunda freshi yanapita kwa kasi barabarani, yakipeleka matunda matamu kutoka Afrika Kusini kwenye supamaketi na masoko sehemu mbali mbali nchini China. “Kwa ushuru wa forodha kushuka kutoka asilimia 10 hadi sifuri, gharama za uagizaji kwa shehena hii ya tufaha imepungua kwa karibu Yuan 20,000," amesema Luo Shengcong, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Usafirishaji wa Mizigo ya Jianchengye ya Shenzhen.
Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika. Tangu Mei 1, China imeanza kutekeleza kikamilifu hatua ya kutoza ushuru-sifuri (zero-tariff) kwa nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia nayo.
"Ushuru-sifuri utavutia kampuni nyingi zaidi za China kuanzisha viwanda barani Afrika; timu za kuunga mkono huduma za ndani kama vile za urejelezaji (recycling), mafunzo ya ujuzi, na matengenezo ya baada ya mauzo nazo zitafuata, na hivyo kuunda mnyororo wa ikolojia unaozidi kuwa kamili." Wang Haiguang, Naibu Meneja Mkuu wa Idara ya Biashara ya Nje wa kampuni ya Zhejiang Zhongzhe New Energy amesema, akieleza matumaini makubwa juu ya fursa kubwa ya ukuaji katika soko la nishati mpya barani Afrika.
Takwimu za forodha zinaonyesha kwamba katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu, biashara ya kuagiza na kuuza nje ya China kwa nchi za Afrika ilifikia jumla ya Yuan trilioni 1.14, ikizidi kiasi cha Yuan trilioni 1 kwa mara ya kwanza katika kipindi kama hicho – ambayo inawakilisha ongezeko la asilimia 18.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Mafanikio hayo mapya katika biashara kati ya China na Afrika yanaonyesha hatua madhubuti ambazo China inapiga katika kupanua ufunguaji mlango wa kiwango cha juu.
Mapema mwaka 2005, China ilianza kutoa upendeleo wa kutoza ushuru-sifuri kwa bidhaa mahsusi kutoka nchi zilizo nyuma kimaendeleo (LDCs); tangu wakati huo, wigo wa bidhaa zinazostahiki, nchi zinazonufaika, na hatua husika za kurahisisha biashara vimekuwa vikipanuliwa kila mara.
Mwaka huu, China imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani kutekeleza utozaji ushuru-sifuri wa upande mmoja kwa nchi zote za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia nayo, vilevile kwa nchi zote zilizo nyuma kimaendeleo.
Ushuru-sifuri huo utavutia washirika wengine wa kibiashara wa Afrika, ikiwemo China, kuongeza uwekezaji barani Afrika, hali ambayo itaingiza mtaji, teknolojia, vifaa, na utaalamu wa usimamizi, na hivyo kuunda mfumo mpya wa ushirikiano wa mnyororo wa viwanda wenye sifa ya "uzalishaji na usindikaji barani Afrika, ukifuatiwa na kusafirisha kuuza China."
Mafanikio hayo mapya ya biashara kati ya China na Afrika yanatumika kama ushuhuda wa kujitolea kwa China kwa ushirikiano na ufunguaji mlango wa kiuchumi tangu kuanza kwa mwaka huu. China inaendelea kufungua soko lake kwa upana zaidi na kuchangia fursa za maendeleo na dunia. Kuanzia mwezi wa 1 hadi wa 5, jumla ya thamani ya biashara ya kuagiza na kuuza nje bidhaa ya China ilifikia Yuan trilioni 20.68, ikiwa ni ongezeko la 15.3% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana; wakati huohuo kampuni mpya 25,297 zilizowekezwa na mitaji ya kigeni zilianzishwa nchi nzima, ikiwa ni ongezeko la 5.3% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Ushirikiano unachochea ukuaji, wakati ufunguaji mlango unawezesha manufaa kwa pande zote. Katikati ya mabadiliko makubwa katika muundo wa uchumi na biashara duniani, China inaendelea kuingiza nguvu ya kutuliza hali na yenye uhakika kwa dunia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



